MKURUGENZI NEC AAHIDI KUSHIRIKIANA NA WAANDISHI WA HABARI UCHAGUZI MKUU 2020


Mwenyekiti wa Arusha Press Club, Claud Gwandu akimkabidhi cheti cha shukrani Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Dkt Wilson Mahera ikiwa ni utambuzi wa mchango wake kwa wanahabari alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Arusha.
Mkurugenzi wa NEC Dkt Wilson Mahera akisaini kitabu cha wageni
Mkurugenzi wa NEC Dkt Wilson Mahera akisalimiana na baadhi ya waandishi na wanachama wa APC mara baada ya kupokea cheti cha heshima kutoka kwa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha.


Na Mwandishi Wetu, Arusha

MKURUGENZI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt Wilson Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya habari nchini kuelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Akizungumza wakati wa hafla fupi, ya kukabidhiwa cheti cha kutambua ushirikiano wake na waandishi wa habari alipokuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha DC, Dkt Mahera ametoa shukrani kwa waandishi na vyombo vya habari kwa kutangaza na kuandika habari zilizofanywa na halmashauri hiyo.

Hafla ya kumkabidhi cheti cha shukrani imefanyika leo katika ofisi za Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC).

Dkt Mahera amesema Rais Dkt Magufuli alipowateua mwaka 2016 aliwataka wakajenge mahusiano mazuri na waandishi wa habari pamoja na jamii ikiwemo viongozi wa dini na viongozi wa kimila.

“Nikiwa kwenye majukumu yangu ya kikazi niliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi, nipende niwaahidi kwamba hata huku nilipo hivi sasa nitaendeleza ushirikiano na waandishi wa habari katika kuendelea kujenga mahusiano kama tulivyoelekezwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli,”alisema.

“Tumejitahidi sana kadiri ya uwezi wetu kujenga mahusiano na kufanya kazi na waandishi wa habari na kwa kweli waandishi wa habari wa Arusha mlinipa ushirikiano wa kutosha,”.

Dkt Mahera pia amewashukuru waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya IPP MEDIA kwa kujitoa zaidi kwenye kuripoti taarifa za maendeleo katika Halmashauri ya Arusha DC.

“Katika Halmashauri ya Arusha DC tulikuwa na kata 26 na vijiji 68, maeneo yote haya tulifika na waandishi wa magazeti haya na stori zao zilitoka, pia tulikutana na matatizo mbalimbali kama kunyeshewa na mvua na kupigwa na jua lakini hatukata tama kwa kuwa yote tuliyafanya kwa maslahi ya wananchi na taifa letu,”alisema.

Alisema agizo la Rais alilowaagiza wakurugenzi kulitekeleza kuhusiana na kujenga mahusiano na jamii alilitoa Julai 12 mwaka 2016 baada ya kupokea malalamiko mbalimbali wakati akiwa katika kampeni za uchaguzi mwaka 2015.

“Wakati nateuliwa ilinipatia wakati mgumu sana kwa kuwa ilikuwa mara yangu ya kwanza kufanyakazi kwenye serikali za mitaa, rafiki zangu walinikatisha tamaa lakini niliwaeleza wacha nikajaribu na kufanyakazi nilitopewa heshima na Rais, na kwa kweli nilifanikisha,”alisema.

Alisema katika utumishi wake, amegundua kuwa katika Serikali za mitaa kunahitaji wasomi kwa sababu ndio kiungo muhimu cha kupeleka mendeleo kwa wananchi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu alimpongeza kwa kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa NEC na kumuahidi kuwa bado waandishi wataendelea kutosha ushirikiano kwake katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

“Sisi kama waandishi wa habari na kwa niaba ya Chama, tunapenda kukupongeza sana, katika utumishi wako ulijitoa bila kufanya ubaguzi , tutaendelea kukukumbuka kusaidia kupata kiwanja cha klabu, ulipokuwa mkurugenzi tunashukuru sana,”alisema Mwenyekiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post