OFISA TUME YA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA AFARIKI DUNIA


Ofisa wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Getrude Alex (40), amefariki dunia usiku wa Novemba 23, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Novemba 26, 2019 na Tume hiyo imesema Getrude alikutwa na mauti baada ya kupata ajali ya kugongwa na pikipiki Novemba 21, 2019 katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam na kukimbizwa Muhimbili kwa matibabu.

Getrude aliajiriwa na tume Oktoba 18, 2010 kama ofisa uchunguzi mwenye taaluma ya habari na mpaka kifo kinamkuta alikuwa amehudumu katika taasisi hiyo kwa takribani miaka tisa.

Historia yake ya maisha inaonyesha kuwa marehemu alikuwa mama wa watoto watatu wa kiume ambao ni Tupendane, Mbarikiwa na Baraka. Kitaaluma marehemu alikuwa ni msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari (SJMC) mwenye Shahada ya Habari (2007).

Marehemu alizaliwa jijini Mwanza Julai 7, 1979. Alianza masomo shule ya msingi Kirumba (1989-1995), baadaye alichaguliwa na kujiunga Mwanza Sekondari ambapo alimaliza elimu ya kidato cha nne (1996-1999). Kidato cha sita alimaliza katika shule ya Sekondari Tagwa (2000-2003).

Marehemu ataendelea kukumbukwa kwa wema wake, ucheshi, ushirikiano wake kwa watumishi hasa katika mambo ya kijamii na ukarimu. Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post