MBOWE AIOMBA MAHAKAMA APUMZIKE .....AMESEMA ANAUMWA HOMA YA DENGUE, MALARIA NA SHINIKIZO LA DAMU


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,  ameiomba mahakama impe muda aweze kupumzika kutokana na afya yake, ambapo amesema anaumwa homa ya dengue, malaria na shinikizo la damu.


Mbowe alitarajia kutoa utetezi wake kwa kuhojiwa na Upande wa Mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hata hivyo, wakili wa Mbowe, Kibatala amedai kuwa kama mawakili wako tayari kuendelea na kesi lakini shahidi (Mbowe) hali yake siyo nzuri hivyo anaomba mapumziko.

Pia kwa sababu kesi hiyo ni ya jinai pamoja na kuumwa kwake homa ya Dengue, Malaria na Shinikizo la Damu ameona ni muhimu kutii mahakama na kuja kusikiliza kesi hiyo.

“Mshitakiwa aliruhusiwa kutoka hospitali Novemba 22 mwaka huu hivyo anaomba kupumzika kwa sababu hali yake si nzuri. Kwa sababu yeye ni shahidi na anatakiwa kujibu maswali tunaomba ahirisho,” amedai Kibatala.

Akijibu hoja hiyo, Nchimbi amedai wiki iliyopita walipokea taarifa ya kuumwa kwa Mbowe iliyoambatanishwa na vyeti vya matibabu lakini wanaamini kuwa tangu Novemba 22, 2019 mshitakiwa aliporuhusiwa na kwa kuwa hakuna maelekezo mengine ya daktari atakuwa amepumzika vya kutosha na amepona.

Hata hivyo waliomba ahirisho kwa siku ya leo na kesi iendelee kama ilivyopangwa.

Hakimu Simba amesema kuwa afya ya mshitakiwa ni jambo la msingi hivyo ameahirisha kesi hiyo kwa siku mbili ambapo itaendelea Novemba 28, 29 na Desemba 2, 3 na 4, 2019 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post