WANAUME MILIONI 4.4 WAFANYIWA TOHARA TANZANIA

Jumla ya wanaume milioni 4,456,511 wamefanyiwa tohara kinga ya kitabibu tangu 2009 ilipoanza kutolewa hadi kufikia Septemba, 2019 nchini kote.

Hayo yamesemwa na Afisa Mpango kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP), Dk. Sasan Mmbando wakati wa semina ya kuwajengea uelewa wabunge wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Kamati yabkudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na kamati ya Katiba na Sheria kuhusu mpango huo.

Dk. Mmbando alisema kuwa lengo la kwanza la afua hiyo lilikuwa kuwafikia wanaume na vijana milioni 2.8 kufikia Septemba, 2017.

“Hadi kufikia Septemba, 2017 tumeweza kuwafikia milioni 3,303,940 na kuwatahiri,” alisema.

Aidha, alisema katika lengo la pili kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 wana mpango wa kuwafikia wanaume milioni 2.7.

Alisema hadi kufikia Septemba, 2019, tayari wameweza kuwatahiri jumla ya wanaume 1,681,070 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya lengo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inatekelezwa katika mikoa 17 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya HIV na kiwango kidogo cha utahiri nchini.

“Hata hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili kuwa na huduma endelevu na kupunguza matatizo ya njia ya mkojo, mfano UTI, ilianza kutoa huduma ya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60, 2013, kama utafiti wa kujifunzia (pilot study), katika mkoa wa Iringa hadi sasa imefikia mikoa 15 nchini,” alibainisha.

Alisema hadi kufikia Septemba, 2019 jumla ya watoto wachanga 13,603 wametahiriwa.

“Tohara ya watoto wachanga inafanyika katika mikoa 15, Iringa Njombe, Morogoro, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya na Kigoma,” alisema.
Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527