MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE, MAWAZIRI WA ULINZI WA SADC WAKUTANA KUJADILI HALI YA AMANI DRC


Mawaziri wa Mambo ya nchi za Nje pamoja na Mawaziri wa Ulinzi na vyombo vya ulinzi  vya Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) ijulikanao kama DOUBLE TROIKA wamekutana kwa dharura kujadili hali ya kisasa na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha amani katika nchi hiyo.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa dharura wa DOUBLE TROIKA inayojumuisha Troika ya siasa na Troika ya Ulinzi na Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa lengo la mkutano huo wa dharura ni kuweka mikakati itakayosaidia kuimarisha amani nchini Congo DRC na kumaliza migogoro inayotishia ustawi wa nchi hiyo iliyodumu kwa miongo mingi.

Aidha, Waziri Kabudi amebainisha kuwa mkutano huo utasaidia nchi za SADC zenye vikosi vya ulinzi na usalama nchini DRC yaani Tanzania, malawai na Afrika Kusini kuimarisha amani na DRC kwa kufanya tathmini na kukubaliana hatua za kuchukua ili vita na migogoro ya mara kwa mara inayoibuka Nchini Congo DRC ifikie tamati na amani ya kudumu ipatikane.

“Mkutano huu wa leo ni wa Troika ya Siasa na Troika ya ulinzi na usalama ambapo kupitia mkutano huu tunaamini kuwa tutafanya tathimini ya hali ya amani DRC na kukubaliana ni hatua gani za kuchukua,” amesema Prof. Kabudi

Katika hatua nyingine Prof. kabudi ameongeza kuwa ndani ya mwaka huu amani na demokrasia vimezidi kuimarika katika nchi wanachama wa SADC, kutokana na baadhi ya nchi wanachama kuendesha chaguzi za kidemokrasia zilizomalizika kwa amani katika nchi za Msumbiji na Botswana.

Aidha Prof. Kabudi amesema Tanzania na Nchi 16 wanachama wa SADC bado zinaendelea kupaza sauti kwa jumuiya za kimataifa na nchi ambazo zimeiwekea vikwazo Zimbabwe kuviondoa mara moja kutokana na vikwazo hivyo kutokuwa na uhalali jambo linalosababisha mateso kwa raia wan chi hiyo hususani akina mama na watoto .

“Katika hili la Zimbabwe lazima sisi kama SADC tushikamane na kusafiri pamoja ili tufike kwa umoja wetu” Amesema Prof. kabudi.

Awali akitoa hutuba katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC), Stegomena Taxi amesema kuwa ana matumaini makubwa na mkutano huo unaofanyika jijini Dar es salaam utatathimini na kutoa mapendekezo ya muda mfupi na mrefu kuhusu hali ya usalama, amani na siasa katika nchi ya Congo DRC  na ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ili kuhakikisha ukanda huo unakuwa salama na amani

Ameongeza kuwa amani na usalama ni nyenzo mojawapo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na hivyo kupata maendeleo yanayohitajika kwa ajili ya mataifa ya Afrika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527