MWENYEKITI AUAWA AKITATUA MGOGORO WA ARDHI KIJIJINI

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira wilayani Kiteto mkoani Manyara, Engerusi Mikonde (59), ameuawa katika shamba moja akiwa kwenye harakati za kutatua mgogoro wa ardhi ambao unadaiwa kuwa ungeleta madhara kati ya wakulima hao.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augostino Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema uchunguzi unaendelea na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Kiteto.

Mmoja ya wakazi walioshuhudia tukio hilo Daiomoni Nzungu, amesema Mikonde akiwa na kamati ya mazingira kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa wakulima Kijijini hapo, alishambuliwa kwa marungu na mapanga hadi alipokutwa na umauti.

Baadhi ya wananchi wamelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo wakisema kuwa suluhu ya sakata hilo ni kupatikana kwa taarifa ya kina ili sheria ifuate mkondo wake kwa waliohusika.

Migogoro mingi ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto huanza kipindi ambacho wakulima wanaandaa mashamba huku wafugaji wakihitaji maeneo kwaajili ya shughuli za kufugia mifugo yao.
CHANZO - MTANZANIA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527