IDRIS ARIPOTI TENA POLISI MAKOSA YA MTANDAO...ANATUHUMIWA KUSAMBAZA UONGO NA KUJIFANYA RAIS

Na Pamela Chilongola, Mwananchi 
 Mchekeshaji na mshindi wa shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan ameripoti kituo cha polisi kati leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 na kuhojiwa kwa dakika 30 na kutakiwa kuripoti tena Jumatano Novemba 6, 2019.

Jana asubuhi, Idris aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa kwa saa tano na kupekuliwa nyumbani kwake, usiku aliachiwa kwa dhamana akitakiwa kuripoti tena leo saa 2 asubuhi, jambo ambalo amelitekeleza.

“Idris ameripoti kituoni saa 2:00 asubuhi na kuhojiwa kwa dakika 30. Wamechukua simu zake kwa uchunguzi na kutakiwa kuripoti tena Jumatano ijayo (Novemba 6, 2019).”

“Wamemueleza kuwa kosa lake ni kusambaza habari za uongo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao. Kosa la pili ni kujifanya Rais chini ya kifungu cha 15 cha makosa ya mtandao,” amesema, Benedict Ishabakaki ambaye ni mwanasheria wa mchekeshaji huyo.

Jana alipopekuliwa nyumbani kwake polisi walichukua kompyuta mpakato kwa ajili ya uchunguzi, aliporudishwa kituoni kabla ya kupewa dhamana alipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni.

Juzi mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaka Idris kuripoti polisi baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Ilivyokuwa
Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527