WADAI MSINGI WA KIINGEREZA SHULE ZA AWALI SIRI YA USHINDI MADARASA YA JUU

Na Abby Nkungu, Singida.

Imeelezwa kuwa msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza kwa watoto wanaosoma shule za Awali zinazotumia lugha hiyo ni moja ya sababu za wanafunzi wengi wanaotoka katika shule hizo kufanya vyema zaidi kitaaluma kwenye madarasa ya juu. 

Wakizungumza mjini Singida, baadhi ya wazazi wamesema kwa kuwa kiingereza ndio lugha rasmi ya kufundishia masomo yote isipokuwa kiswahili pindi mwanafunzi anapoingia Sekondari, hivyo msingi mzuri wa lugha hiyo kwa wanafunzi wanaotoka "English Medium" imekuwa siri kubwa ya mafanikio yao ikilinganishwa na wanaotoka shule za Serikali.

"Hebu fikiria, mtoto tangu darasa la Awali anafundishwa Kiswahili masomo yote isipokuwa Kiingereza, halafu ghafla akienda Sekondari anakutana na Kiingereza katika masomo yote isipokuwa Kiswahili. Je, unadhani ataweza kumudu vyema?" alihoji Athumani Iddi, mmoja wa wazazi na kuongeza “hiyo ndiyo sababu ya wengi wa wanafunzi kutoka English Medium hufanya vizuri zaidi Sekondari kuliko waliosoma shule za kawaida". 

Mzazi mwingine, Helena Mussa anaona kuwa sababu sio tu msingi wa Kiingereza kuwa mzuri bali pia ni kutokana na shule hizo kuwa makini zaidi katika ufundishaji kwa lengo la kufanya vizuri kwenye mitihani na kuvutia wateja kutokana na kuendeshwa kibiashara. 

Aidha, wametaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na shule hizo kusheheni vifaa changamshi kwa ukuaji na ujengaji ubongo wa mtoto katika umri mdogo; kama vile michoro ya kujifunzia na kufundishia darasani na uwepo wa michezo mbalimbali wakati wa mapumziko hali ambayo ni tofauti kwenye shule za Serikali.

Kutokana na hali hiyo, wengi wa wazazi wameiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa utoaji elimu katika shule zake kuanzia madarasa ya Awali ili kama mtoto anafundishwa Kiswahili aendelee nacho hadi elimu ya juu; vinginevyo wanafunzi wote wawe wanaanza masomo yao kwa lugha ya Kiingereza kuanzia madarasa ya Awali. 

Wanadai kuwa hiyo itaondoa changamoto inayowakumba watoto wanaotoka shule za msingi za Serikali lakini wakifika Sekondari wanakutana na lugha ya Kiingereza kwa wingi.

Ofisa elimu (Elimu ya Watu Wazima) mkoa wa Singida, Suleiman Nkondo anakubaliana na dhana hiyo ingawa anasema kuna sababu nyingine za ziada kama vile kujituma kupindukia katika ufundishaji na baadhi ya Wamiliki wa shule hizo kutumia njia za 'ujanja ujanja' kwa nia ya kutaka shule zao zionekane bora zaidi.

Nao, Wataalam wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wanasema Lugha ya Kiingereza ni nyenzo muhimu ya mawasiliano katika elimu hasa elimu ya sekondari; hivyo kuijua kunaweza kukawa na mchango mkubwa katika kujifunza ingawa wanasisitiza ufaulu hutegemea vitu vingi, ikiwemo umahiri wa lugha. 

Kwa mujibu wa Matokeo ya Mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi Manispaa ya Singida (yenye idadi kubwa ya shule za English Medium), kati ya shule 10 bora mwaka jana na mwaka huu, nafasi tano za juu zimechukuliwa na Shule zinazofundisha Kiingereza. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527