MRADI WA KIWANDA KIKUBWA CHA DAWA TANZANIA WAVUTIA WAWEKEZAJI WA KIMKAKATI AFRIKA KUSINI | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, November 12, 2019

MRADI WA KIWANDA KIKUBWA CHA DAWA TANZANIA WAVUTIA WAWEKEZAJI WA KIMKAKATI AFRIKA KUSINI

  Malunde       Tuesday, November 12, 2019

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kulia) akizungumza na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Alex Mubiru, kando ya Kongamano la Jukwaa la Wawekezaji Afrika (Africa Investment Forum), unaoendelea Jijini Johannesburg, Afrika Kusini
Msimamizi wa Dawati la Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Said Nyenge (wa pili kulia) akimweleza Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika Dkt. Alex Mubiru (kulia) kuhusu miradi ya kipaumbele iliyowasilishwa na Serikali kwenye Kongamano la Jukwaa la Uwekezaji Afrika), linalofanyika Johannesburg, Afrika Kusini. Kulia ni Bw. Frank Sanga kutoka AfDB na wa pili kulia ni Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipangp Bw. Abel Philip.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Abubakar Ndwata, akimweleza mwekezaji kutoka Kampuni ya Burhani Engineers kutoka Zoher Pirbhai kutoka nchini Kenya kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania, wakati wa Kongamano la Jukwaaa la uwekezaji la Afrika, linalofanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (aliyeipa mgongo kamera kushoto) akizungumza na wawekezaji wa kimkakati walioonesha nia ya kuwekeza kwenye Mradi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa chenye thamani ya dola za Marekani milioni 408, kutoka nchi za Korea, Uturuki na taasisi za fedha za kimataifa, wakati wa Jukwaa la Africa Investment Forum), unaoendelea Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Baadhi ya wawekezaji wa kimkakati kutoka nchini Korea, Uturuki na Taasisi za Fedha za Kimataifa, wakielezea nia yao ya kuwekeza kwenye Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha dawa nchini Tanzania unaotarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 408, walipokutana na kufanya kikao na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

**

Na Benny Mwaipaja, WFM, Johannesburg 

Tanzania imewasilisha miradi 13 ya Kipaumbele kwa wawekezaji wa kimkakati wanaoshiriki kongamano la Jukwaa la Uwekezaji Jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango anayemwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Jukwaa hilo, amesema Mradi wa Ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa mchanganyiko kitakachogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 408 umewavutia wawekezaji wengi.

Amewataja wawekezaji waliovutiwa na mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachojengwa Kibaha mkoani Pwani, kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya aina 230 za dawa kwamba wanatoka nchi za Korea, Uturuki, taasisi za fedha za kimataifa na kwamba hadi kufika mapema mwakani (2020) mwekezaji mmoja au zaidi watakuwa wamepatikana kwa ajili ya kuanza kujenga mradi huo.

"Pamoja na kupunguza tatizo la uhaba wa dawa na dawa bandia zinazoingizwa nchini, kiwanda hiki pia kitazalisha ajira kwa watanzania" alisema Dkt. Mpango. 

Dkt. Mpango amesema Serikali inatenga zaidi ya sh bilioni 230 kwenye Bajeti kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa huku mahitaji halisi ya dawa nchini ni takriban shilingi trilioni 1.4 ndio maana mkazo umewekwa kwenye ujenzi wa kiwanda hicho kitakachotatua changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.

Alifafanua kuwa miradi mingine 12 iliyowasilishwa mbele ya wawekezaji hao iko katika hatua za maandalizi na iko katika sekta za Nishati ya umeme unaotumia nguvu ya maji, viwanda vya kuchakata pamba ili kuiongezea thamani na hatimaye kuzalisha nguo, ambavyo vinaendana na dhamira ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka Bohari ya Dawa ya Taifa Mhandisi Fredrick Pondamali ameeleza kuwa usanifu wa mradi huo wa kiwanda cha kuzalisha dawa mchanganyiko umekamilika pamoja na viwanda vingine viwili zaidi vinavyotafutiwa wawekezaji.

Alisema kuwa mradi wa kiwanda cha kuzalisha dawa ulichaguliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa lengo la kuupeleka mbele ya wawekezaji ili uweze kupata fedha kutokana na umuhimu wake kwa Tanzania na nchi jirani.

Jukwaa hilo la Uwekezaji Afrika linalofanyika kwa mwaka wa pili sasa limeandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali ambapo mwaka huu limevuta wawekezaji wa kimkakati zaidi ya 4000 kutoka kila pembe ya dunia ikiwa na lengo la kuongeza uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi katika nchi za Bara la Afrika.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post