MWANAFUNZI AFARIKI AKIJIANDAA KUFANYA MTIHANI WA BIOLOJIA KIDATO CHA NNE 2019

Mwanafunzi aliyekuwa akiendelea na mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mwemage Kata Ibwera Bukoba Vijijini, Pasficus Medichades, amefariki dunia kutokana na kukosa hewa ya Oksijeni katika chumba alimokuwa akiishi.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alisema kuwa mwanafunzi huyo alikutwa na mauti usiku wa kuamkia Jumamosi, na kwamba alikuwa amejifungia ndani akiendelea kujisomea ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mtihani.

Kamanda Malimi alisema inahofiwa wakati akiendelea kujisomea alipitiwa na usingizi na wakati huo kulikuwa na jiko la mkaa ndani likiwaka. 

“Kwa bahati mbaya alifunga mlango na madirisha, kwa hiyo alikosa hewa akawa amefariki," alisema.

Mkuu wa shule hiyo, Leonard Ndyakowa, alisema mwanafunzi wake aliyekuwa akiendelea na mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, na kueleza kuwa alikuwa akiishi na mama yake mzazi, ambaye siku ya tukio aliondoka kwenda katika makazi yake mengine na kumwacha mtoto wake peke yake. 

"Ni tukio la kweli, lakini limetokea nje ya mazingira ya shule, inaonekana mwanafunzi huyo alikuwa akipika ndani, akajilaza pembeni na inaonekana alikuwa akijikumbushia masomo kwa kujisomea akapitiwa na usingizi, na ndo kikawa kifo chake,” na kuongeza:

"Alikuwa amebakiza mtihani mmoja tu Biolojia paper 2, lakini Mungu akamchukua, tulishtushwa sana na taarifa za kifo chake, lakini hatuna la kufanya, ni mapenzi ya Mungu.”

"Ni tukio la kwanza kutokea katika mtihani huu, limetusikitisha lakini baada ya kutokea mwanafunzi walipata mshtuko na baadae walirejea katika vyumba vya mtihani na kuendelea na mitihani yao, alisema Ofisa Elimu (sekondari) Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Deo Chacha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post