IGP SIRRO: RUDISHENI MAHARI, WATOTO WA KIKE SIO MITAJI


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka wazazi wote na walezi Mkoani Mara walioozesha watoto wadogo wakiwemo wanafunzi kurudisha ng’ombe walizopokea kama mahari vingenevyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na watafungwa jela.


“Baba wa Tanzania hauko juu ya sheria ukimpiga mkeo ni kosa la jinai ukimuozesha mwanao kabla ya umri ni kosa utashughulikiwa tu, lazima tufunge watu sasa hata kama wazazi wamekubaliana tutawagonga kwa mujibu wa sheria”amesema

Sirro ametoa agizo hilo Wilayani Bunda Mkoani mara wakati wa uzinduzi wa madawati ya jinsia Mkoani humo ambapo akiwa Bunda ametoa agizo kwa wazazi wote na walezi kuhakikisha wanawarudisha watoto wote waliowaozesha na warudishe mahari kama wanataka mali wazitafute kwa kufanyakazi na siyo kufanya watoto wa kike mtaji.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi ameendeleza kauli mbiu yake ya polisi kutumia nguvu ya kadri kwa wanaume wote nchini wanaopiga wake zao ili kukomesha vitendo vya ukatili ambavyo amesema Mkoa wa Mara unaongoza kwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

“Bahati mbaya sana mimi ni IGP na natokea Mkoa huu sasa kuanzia sasa huu ukatili haukubaliki madawati haya ya jinsia yatafanyakazi saa ishirini na nne mwana mama ukipigwa muda wowote wewe nenda kituoni utapata huduma na huyo aliyekupiga atapata huduma anayostahili”ameongeza Sirro

Aidha amewaomba viongozi wa madhehebu ya dini wafanye kazi ya doria ya kiroho kwa waumini wao  ili waachane na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mkuu wa wilaya ya Bunda Bi Lidya Bupilipili akimkaribisha IGP wilayani hapa ameeleza kuwa mbali na ukatili kwa watoto lakini kuna changamoto ya wanafunzi wa kike kutumia uzazi wa mpango wakati bado wanasoma.

Amesema wazazi wamewekeza kwenye mambo ambayo hayana tija badala ya kuwekeza kwenye elimu ndiyo maana mmomonyoko wa maadili ni mkubwa.

“Sijawahi kushuhudia katika kesi nnazopokea ofisini kwangu baba amekatwa mapanga lakini kila siku ni wanawake tu na jambo la kusikitisha kuna baadhi ya viongozi wa vijiji hawalichukulii kwa uzito ukatili huu”amesema mkuu  wa wilaya

Mkurugenzi wa jukwaa la Utu wa Mtoto CDF bw Koshuma Mtengeti amewataka wana Mara kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na wasiogope kwenda kutoa ushahidi wanapohitajika.

Ameongeza kuwa kamati za ulinzi na usalama zinapaswa kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu kuanzia ngazi ya chini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527