ALIYEIKAMATA NDEGE YA ATCL AFRIKA KUSINI KAIKAMATA TENA HUKO CANADA

Ndege  nyingine ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombadier ambayo ilikuwa ikijiandaa kuja Tanzania imekamatwa nchini Canada, ambapo aliyefanya hivyo ni yuleyule (Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini) ambaye aliikamata ndege kama hiyo nchini Afrika Kusini miezi michache iliyopita lakini Serikali ya Tanzania ikamshinda mahakamani.


Hayo yamesemwa leo, Jumamosi Novemba 23, 2019 na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati akihutubia baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha mabalozi wateule watano watakaoiwakilisha Tanzania nchi mbalimbali ambapo hafla hiyo ya imefanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.

Mabalozi walioapishwa leo Ikulu Dodoma ni;
  1. Mhe. Mej. Jen. Mstaafu Asleim Bahati, Balozi wa Tanzania Misri
  2. Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi nchini Ubelgijji
  3. Mhe. Mohammed Mtonga, Balozi wa Tanzania, UAE
  4. Mhe. Jilly Maleko, Balozi nchini Burundi
  5. Mhe. Ali Mwadini, Balozi nchini Saudi Arabia.

Profesa Kabudi amesema kuendelea kwa vitendo hivyo ni hujuma za mabeberu wasiofurahishwa na maendeleo nchini.
 


“Tulikwenda mahakamani tukamshinda (Afrika Kusini) akakata rufaa na wiki iliyopita tukamshinda tena, huyohuyo sasa amekimbilia Canada amekamata ndege ya Bombardier Q400 ambayo ilikuwa ifike nchini.

“Jambo linalosikitisha ndege zilizokuwa zinatoka Marekani aina ya Dreamliner mbili hazikukamatwa zimefika lakini kila ndege inapotakiwa kuondoka Canada tunashangaa hao matapeli wanajuaje na ndege zinakamatwa.” Amesema Profesa Kabudi.


 
Amesema Balozi wa Tanzania nchini Canada aliitwa nchini na kuelezwa jinsi nchi isivyofurahishwa na kukamatwa kwa ndege zake kila zinapokaribia kuja kuondoka nchini humo.
 


“Jana nimemuita Balozi wa Canada, nimeongea naye kinagaubaga na kumwambia, haturidhishwi na tumechukizwa na tabia inayoendelea ya ndege zetu kukamatwa kila zinapotaka kutoka Canada, Mheshimiwa rais tunafikiri kukushauri kuhusu suala la kununua ndege Canada, si wao pekee wanaotengeneza ndege, hata Brazil wanatengeneza.

“Wanasingizia hali ya hewa, wanasimamisha safari zake, kisha wanaikamata. Kule Afrika Kusini tulimshinda kesi ya msingi na rufaa sasa hivi amekimbilia Canada, tayari tumeshapata wanasheria kule Canada na taratibu zote za kutetea ndege yetu zimeanza.“Hoja yetu kubwa ni kuwaeleza watu wa Canada kwamba amekenda kwenye mahakama za nje ameshindwa na sasa amekimbilia Canada. Sasa tumeelewa kuwa kila unapoleta maendeleo wapo mabeberu wa nje na wengine wa ndani wanaotuhujumu. Wanakesha wakiunguruma ili wairarue nchi hii,” amesema Prof. Kabudi.

Kushikiliwa kwa ndege hiyo kunarejesha kumbukumbu ya ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 iliyozuiwa nchini Canada mwaka 2017 kutokana na madai ya Sh87.3 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post