WAZIRI MKUU: VIWANDA 4,000 VIMEJENGWA CHINI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO


Waziri  Mkuu  Kassim Majaliwa amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa na hivyo kufanya sekta hiyo kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 8.05 na kutoa ajira 306,180 mwaka 2018.

Akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli jana Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa tuzo za Rais kwa wazalishaji bora wa viwandani (PMAYA)  mwaka  2018 alisema  kutokana na sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa, Serikali itavipa kipaumbele viwanda vinavyotumia malighafi za ndani zaidi.

Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) ilishirikisha makampuni 61 ambapo mshindi wa jumla ilikuwa ni kampuni ya Hanspaul iliyoko mkoani Arusha.

“Sekta ya viwanda imeendelea kuongeza pato la taifa na mwaka 2018 imeongezeka kwa asilimia 8.05  tofauti na mwaka  2017ambayo ilikuwa asilimia 7.67, Aidha, katika kipindi cha mwaka 2018 Sekta ya viwanda ilichangia asilimia 18.1 ya mauzo yote ya nje, ikilinganishwa na asilimia 15 mwaka 2017 pia, takwimu zinaonyesha kwamba katika mwaka 2018 Sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180 ikilinganishwa na ajira 280,899 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 9.

“Mkakati wetu wa kuendeleza viwanda nchini kipaumbele kimewekwa katika viwanda ambavyo vinatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini, tunahitaji kupunguza uuzaji wa mazao yetu ya kilimo, misitu, madini na maliasili nje ya nchi yetu yakiwa ghafi, hali kadhalika tunalenga kutumia rasilimali zilizopo nchini kuzalisha  bidhaa ambazo  hivi sasa tunaziagiza kutoka nje.

“Shabaha yetu ni kutosheleza mahitaji ya ndani ya bidhaa za viwandani, na kuwa na ziada tutakayouza nje  ya nchi ili kupata fedha za kigeni, kukuza ajira na kuongeza kipato cha Watanzania kwa ujumla,yote haya yatawezekana kama tutatengeneza miundombinu kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa bora,”alisema Majaliwa.

Alisema ili kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa viwanda Serikali haina budi kuhahakikisha ukuaji wa uchumi unafikia asilimia 12 kwa mwaka.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527