NAIBU WAZIRI WA FEDHA DKT. KIJAJI AIAGIZA TRA KUWEKA MIFUMO IMARA YA UKUSANYAJI MAPATO

Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka mifumo imara ambayo itamtambua kila mfanyabiashara na bidhaa anayouza ili kuweza kukusanya kodi stahiki na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.

Mhe. Kijaji aliyasema hayo kwa viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa Mikoa ya Kodi ya Ilala na Kariakoo, wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Mamlaka hiyo inayoendelea  Jijini Dar es Salaam.  

Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba inavuka lengo la makusanyo iliyojiwekea ili kuweza kumsaidia Mhe. Rais DKt. John Pombe Magufuli, atekeleze majukumu yake kwa ufanisi na kulifikisha Taifa pale alipodhamiria.

“Naiagiza Mamlaka kuanza zoezi la kukagua watumiaji wote wa mashine za utoaji risiti za kieletroniki  (EFD) hasa kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti na kwa kufanya hivyo itasaidia  kuongeza makusanyo na kupelekea Taifa letu kujiendesha kupitia  fedha zetu wenyewe kwa kuwa hakuna Taifa huru bila mapato’’ alisisitiza Dkt. Kijaji

Aliwataka Maafisa wa TRA kutokaa ofisini badala yake wawatembelea wafanyabiashara ili kuhakiki matumizi ya mashine za utoaji wa risiti za kieletroniki (EFD).

Awali Meneja wa Ofisi ya Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Bw. Alex Katundu alimueleza Mhe. Kijaji kuwa Mkoa wake wa kikodi una jumla ya wafanyabiashara waliosajiliwa na Mamlaka hiyo 22,279 na kati ya hao wafanyabiashara 16,068 wanatumia mashine za EFD.

Alisema Mkoa wa kodi wa Kariakoo kwa mwaka 2018/19 walidhamiria kukusanya shilingi bilioni 138.66 lakini walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 109 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya malengo waliyojiwekea.

Katika Mkoa wa kikodi wa Ilala, Kaimu Meneja Bw. Steven Kuzeni amesema katika kuhakikisha Mkoa wake unakusanya ipasavyo kodi ya Majengo, wamedhamiria kusajili majengo yote yanayozunguka Mkoa huo wa kikodi na hadi sasa wameshasajili majengo katika kata 26 kati ya kata 32 zilizopo katika eneo lake.

“Ofisi yangu kwa mwaka 2019/20 ina mkakati kabambe wa kuhakikisha inaongeza idadi ya walipa kodi ya mapato na wale wa ongezeko la thamani (VAT)” Aliongeza Bw. Kuzeni.

Katika hatua nyingine Kijaji amewapongeza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwezi Septemba ambapo imekusanya sh. trilioni 1.76, kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa tangu nchi ipate uhuru na kuwahimiza kukaa pamoja na Taasisi zote zinazofanya kazi kwa karibu na Mamlaka hiyo  ili kuona ni kipi kinaweza kuboreshwa zaidi ili kuwapa fursa Watanzania kulipa kodi bila Serikali kuwalazimisha.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527