MBWA,PAKA 890 WAPEWA CHANJO BURE KAHAMA

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Zaidi ya mbwa na paka 890 wamepewa chanjo dhidi ya kuzuia kichaa cha mbwa wilayani kahama mkoani Shinyanga katika zoezi maalumu la chanjo hiyo inayotolewa bure na shirika la kuhudumia wanyama Tanazania (TAPO).

Akizungumza katika Maadhidhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani ambayo hufanyika kila mwaka Septemba 28,2019 yaliyofanyika wilayani humo, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Emmanuel Nangayi alisema chanjo hiyo ni muhimu sana kwa ajili ya kuzuia ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni miongoni mwa magonjwa hatari ambayo hayana tiba na unaua kwa haraka hivyo ni vyema wakajitokeza kuwaleta mbwa wao na paka ili wapatiwe chanjo hiyo bure.

“Kinga hii ni ya mwaka mmoja na mbwa au paka asipochanjwa ni rahisi kupata ugonjwa huu nichukue fursa hii kuwaomba wananchi wa kahama kuhakikisha wanyama wao wanapewa chanjo hiyo”,alisema Nangayi.

Kwa upande wake Mtaalamu wa wanyama kutoka shirika la TAPO, George Master alisema ni vyema wananchi wakaacha ufugaji wa mbwa nap aka kiholela kwa kutowapatia matunzo maalumu ikiwa ni pamoja na kuwapatia chanjo na chakula hali ambayo inasababisha wanyama hao kuzurura ovyo.

Alisema ni vyema wafugaji wote wa mifugo hiyo wanapokuwa na tatizo wasisite kuwasiliana na shirika la TAPO ili wapatiwe elimu juu ya ufugaji wa kisasa wa wanyama mbalimbali wafugwao majumbani.
Mtaalamu wa wanyama kutoka shirika la TAPO, George Master akizungumza kuhusu chanjo ya mbwa na paka
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Emmanuel Nangayi akizungumza kuhusu chanjo kwa mbwa na paka

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527