ASKOFU AONYA MAKASISI NA MASHEMASI WANAOTUMIA CHUMVI NA MAFUTA KUHADAA WAUMINI

Askofu Ezekiel Yona 
Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Makasisi na Mashemasi wa kanisa la Moravian jimbo la Magharibi wametakiwa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa maombi ambao wamekuwa wakitumia chumvi na maji pamoja na mafuta kuwahadaa waumini wanaohitaji maombi badala yake wafuate maelekezo ya Yesu Kristo aliyokuwa akiyatumia katika maombi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Askofu wa kanisa la Moravian Ezekiel Yona wa Jimbo la Magharibi katika hafla maalum ya kuliweka wakfu wa jengo jipya la kanisa la Moravian la Kahama Mjini pamoja na kuwasimika mashemasi 17.

Askofu Yona amewataka Makasisi hao kuepuka maombezi yanayokwenda kinyume na taratibu mungu na badala yake wafuate taratibu na miongozo ya kanisa hilo ambayo ni mafundisho ya kristo ili kuendelea kutangaza habari njema kwa watu wote.

“Kinachonitatanisha ni kitu kimoja sasa hivi wapo baadhi ya watoa huduma za maombi wanaowanywesha mafuta waumini wao na kisha wanaanguka chini na baadaye wanawaombea na kuamka,vitendo hivi msivifanye na havikubaliki katika kanisa la Mungu”,alisema Askofu Yona.

Katika hatua nyingine Askofu Yona amewataka Makasisi hao kuendelea kuliombea Taifa ili amani iendelee kudumu sambamba na kumwombea Rais John Pombe Magufuli ili aendelee kuwatetea wanyonge sanjari na kurudisha nidhamu serikalini kwa kusimamia rasilimali za nchi.

Nao baadhi ya Makasisi wapya waliopewa daraja hilo, Emanuel Sangosango kutoka Kanisa la Moravian kituo cha (SAUT)Mwanza na Yona Mbogo wa kanisa la Moravian kituo Singida wameahidi kuwa waaminifu katika utoaji wa huduma kwa waumini wao pamoja na kujiepusha na maombi yasiyofuata mafundisho ya Mungu.

Wamesema wapo baadhi ya wachungaji ambao wanatumia vitu kama vile mafuta, chumvi na maji kuwahadaa waumini wao ili kupona magonjwa mbalimbali waliyonayo jambo ambalo sio la kweli na kutoa rai kwa waumini kuepuka maombi ya namna hiyo.
Askofu wa kanisa la Moravian Ezekiel Yona wa Jimbo la Magharibi akizungumza na waumini wa kanisa la morian la mjni Kahama
Askofu wa kanisa la Morovian Ezekiel Yona wa Jimbo la Magharibi akiwawekea mikono makasisi wapya aliowasimika jana
Baadhi ya makasisi wakiwa wanasikiliza mahubiri ya Askofu Yona
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wakiwa wanaendelea kumsikiliza Askofu Yona

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527