WAZIRI LUGOLA KUTATUA KERO ZA WAMILIKI, WAENDESHA VYOMBO VYA MOTO KUPITIA BONANZA KUBWA LA VIJANA MKOANI DODOMA KESHO

Na Mwandishi Wetu, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza kubwa la Vijana litakalofanyika Chang’ombe jijini Dodoma, kesho.

Bonanza hilo, pia litashirikisha wananchi mbalimbali wakiwemo wamiliki na waendesha vyombo vya moto kutoka Wilaya zote za Mkoa huo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, jijini Dodoma leo, Waziri Lugola alisema amealikwa na viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuwa mgeni rasmi ambao ndio waratibu wa Bonanza hilo.

Lugola alisema amepewa taarifa na uongozi wa UVCCM Mkoa, kuwa wamejipanga vizuri na pia Bonanza hilo litaambatana na michezo mbalimbali na burudani kutoka kwa wasanii wa miondoko ya kizazi kipya.

“Kupitia mkutano huo wa Dodoma, nitalenga kuwahabarisha vijana wote na wananchi kwa ujumla hapa nchini, kuhusu mafanikio ya Serikali katika kuwasaidia vijana kupambana na umaskini, na kutatua tatizo la ajira pasipo kunyanyaswa kwa kujua au kwakutokujua kwa vyombo vya ulinzi na usalama hususani jeshi la polisi, pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali,” alisema Lugola.

Alisema vijana ni nguzo ya taifa, hivyo Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na inawathamini katika mazingira yao ya kujipatia kipato ikilenga kuwapa nafasi mbalimbali ili waweze kupata mafanikio zaidi.

“Mwezi uliopita nilikutana na wamiliki na waendesha bodaboda na bajaj zaidi ya 2000 mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro, nilitoa mwarobaini wa kero zao, ambazo nyingi zaidi zilihusu Manispaa ya Moshi kutowatendea vema katika maeneo mbalimbali ya maegesho ya vyombo vyao vya moto, pamoja na kero nyingine zilizowahusu baadhi ya askari wangu wa kikosi cha usalama barabarani ambapo vijana hao waliwalalamikia,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Billy Chidagwa alisema Bonanza hilo litaacha historia katika mkoa huo kutokana na maandalizi yao waliyoyafanya katika kufanikisha vijana mkoani humo wanakutana pamoja na kero zao kutatuliwa.

Chidagwa alisema vijana mbalimbali watakuwepo katika tukio hilo, hasa wanaotumia vyombo vya moto mbalimbali vikiwemo Bajaj, Bodaboda na waendesha daladala kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.

“Tumejipanga vizuri kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge wa Vijana, Mbunge wetu wa Jimbo, viongozi wa chama, tunaamnini uwepo wao kutakuwa na tija kufanikisha tukio hili ambalo maandalizi yake ni ya muda mrefu, na tayari yamekamilika,” alisema Chidagwa.

Alisema Bonanza hilo litaambatana na michezo mbalimbali, ambapo kwa upande wa mpira wa miguu, timu ya bodaboda itacheza na timu ya Askari Polisi mkoani Dodoma.

“Vijana njooni kwa wingi kesho jumapili tarehe 22 mwezi huu wa tisa pale Chang’ombe ili tufurahi kwa pamoja na kumsikiliza mgeni wetu rasmi, ambaye ni Waziri Lugola atakapotatua kero zetu na kutuonyeshea njia ya mafanikio zaidi katika Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli,” alisema Chidagwa.

Waziri Lugola ambaye alikuwa mkoani Arusha kikazi, amewasili leo jijini Dodoma kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya vijana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527