BALOZI IDDI: TAASISI ZIBORESHE MIFUMO YA KUKUSANYA MAPATO YA SERIKALI


Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akisikiliza kwa makini maelezo ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu kuhusu namna watuhumiwa wa makosa barabarani wanaokamatwa kwa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) wanavyolipia faini zao kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Maduhuli ya Serikali (GePG) katika banda la Serikali Na. 26 kwenye Mkutano wa Mawaziri Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, Jijini Dar es Salaam.

Na Farida Ramadhani, WFM, Dar es Salaam

Taasisi za Serikali zinazotumia mifumo ya kielektroniki zametakiwa kuhakikisha zinaanzisha mfumo wa kuziwezesha kuona taarifa za kila taasisi pindi watakapo huisha mifumo hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi alipotembelea banda la Serikali Na. 26 la mifumo ya kielektroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali (GePG), Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) na Mfumo wa Taarifa za Mali zilizopote (Los Report System) katika Mkutano wa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa.

Balozi Iddi ambaye alifunga mkutano huo, alisema kitendo cha taasisi kuweza kuona taarifa kutoka taasisi nyingine kutarahisisha kazi na kuongeza ufanisi wa Serikali katika kuhudumia wananchi.

“Kama GePG inarahisisha malipo kwa taasisi zote ni vema kukawa na mfumo wa kuziwezesha taasisi hizo hasa zinazotegemeana kuweza kushirikishana taarifa, kama mtu akienda TRA kuhuisha leseni na anadaiwa na Trafiki basi mfumo uoneshe kuwa anadaiwa moja kwa moja”, alisema.

Aidha Balozi Iddi alipongeza mifumo ya GePG, TMS na ule wa taarifa za mali zilopotea na kusema kuwa mifumo hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na imeanzishwa wakati muafaka.

Alisema kuwepo kwa mifumo hii kunaiwezesha Serikali kupata mapato ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumzia mfumo wa GePG Mkuu wa Uendeshaji wa Mfumo huo, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Basil Baligumya, alisema mfumo umeunganisha taasisi zote za Serikali ambapo kila malipo ya taasisi hizo hupitia katika mfumo huo.

Alisema mfumo huo umeongeza makusanyo ya Serikali, umedhibiti fedha za umma, umeongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, pamoja na kuongeza usahihi wa taarifa za mapato.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu alisema kuwa mfumo wa TMS unasaidia kudhibiti makosa ya barabarani kwa kuwakamata wahalifu wote wa makosa hayo kwa kuwa mfumo huo unawezesha kuona watu wote wanaodaiwa tozo za makosa barabarani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527