SHULE YA JAMIA KUWABURUZA MAHAKAMANI WAZAZI WASIOLIPA MICHANGO YA SHULE


Mgeni rasmi Mhandisi  Nasir Chakindo akizungumza wakati wa mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Jamia English Medium Nursery and Primary School.


Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog 
Wazazi na walezi wa wahitimu wa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2019 katika shule ya msingi Jamia English Medium Nursery and Primary School iliyopo katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wametakiwa kumaliza deni la shilingi milioni saba wanalodaiwa kutokana na ununuzi wa gari la shule na kuwalipia ada wanafunzi la sivyo watawafikish mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 4, 2019 na mwenyekiti wa bodi ya shule ambaye pia ni Sheikh wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta wakati wa mahafali ya shule ya msingi Jamia English Medium Nursery and Primary School wakati akielezea maendeleo ya shule hiyo.

Sheikh Kichwabuta amesema baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakipigiwa simu mara kwa mara na wengine kuandikiwa barua zinazowahimiza kukamilisha deni hilo na kuwalipia ada watoto lakini wazazi hao wamekuwa wakikaidi.

Akielezea kuhusu gari la shule amesema madhumuni ya kuletwa kwa gari hilo shuleni hapo ilikuwa ni kuwasaidia watoto wanaoenda shule na kurudi nyumbani baada ya masomo kutokana na wanafuzi hao kupata adha kubwa ikiwemo jua kali,umbali mrefu na mvua lakini wazazi wameshindwa kumalizia kulipa deni la shilingi milioni saba la gari hiyo lililonuliwa ili kuwasaidia wanafunzi kuwahi kufika shuleni.

"Deni la gari ni milioni saba,mwenye gari anazitaka,akilichukua mtafanyeje?..Halafu kibaya zaidi tumepata gari hawataki kuipanda gari,gari inaenda Rwamishenye na mwanafunzi mmoja,wengine wanakanyaga kwa miguu...kwanini hatubadiliki siye,sisi kazi yetu tunafanya lakini nyingi hamtufanyii mnayopaswa kufanya",ameeleza.

 Mwenyekiti huyo wa bodi ya shule pia alieleza kusikitishwa na uchangiaji hafifu wa ada ya shule hali inayochangia shule hiyo kuendelea kukabiliwa na changamoto inayosababisha wakati mwingine walimu kuvunjika moyo licha ya jitihada kubwa wanazofanya kuongeza ufaulu wa wanafunzi shuleni.

"Mwalimu anadai,NSSF inadai,kazi anadai,Mtoto mtoto anasoma mwaka hadi mwaka mzazi halipi ada,na sisi hatuwafukuzi watoto hawa kwa sababu hawana makosa....

"Mimi siwezi kupigwa presha bure, hawa wanafunzi wanamaliza mwaka mzima mzazi analipa laki moja tangu Januari hadi Januari. Tumeandika barua za kuwaita mara kwa mara,wazazi kulipa michango hiyo lakini wazazi hamkutii,tumewaita mje tuzungumze mmekataa kuja....Sasa tunawapeleka mahakamani, mtuletee fedha bwana...

"Tumekaa hapa tumeifanya hii shule ya bure,mpaka leo tunapozungumza tunadai tangu darasa la chekechea hadi darasa la saba wanadaiwa zaidi ya shilingi milioni 81...hii shule itafungwa,mwakani mzazi ambaye hatalipa mtoto wake hatutampokea,shule zingine hakuna kitu kama hiki" amesema.

Kwa upande wao baadhi ya wazazi wa wahitimu hao ambao hwakupenda majina yao yatajwe wameiomba shule hiyo kuwasamehe ili waanze kulipa kidogo kidogo.

Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Nuriat Nuru amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo ulipaji hafifu wa ada ya shule kwa wazazi na  chumba maalumu cha kujisitiri kwa watoto wa kike.

Hata hivyo wahitimu hao wametoa pongezi kwa uongozi wa shule hiyo kwa kuwapatia elimu nzuri yenye maadili na kuwaomba wazazi wao kuona umuhimu wa kuchangia maendeleo ya shule.

Akijibu kuhusu deni la shilingi milioni 7 la gari hilo, mgeni rasmi katika mahafali hayo Mhandisi  Nasir Chakindo, amechangia shilingi laki 3 na kuungwa mkono na wadau mbalimbali waliochangia shilingi laki 7 huku akiwataka wazazi hao kuchangia maendeleo ya shule ili kutowavunja moyo walimu.
Mwenyekiti wa bodi ya shule ya msingi Jamia English Medium Nursery and Primary School ambaye pia ni Sheikh wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta akizungumza wakati wa mahafali ya darasa la saba leo
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Jamia English Medium Nursery and Primary School, Bi Nuriat Nuru akizungumza wakati wa mahafali ya darasa la saba

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post