WATUHUMIWA WA WIZI WA DHAHABU WAFIKISHWA MAHAKAMANI JIJINI MBEYA

Na Tito Mselem, Mbeya
Watuhumiwa 10 wanaodaiwa kuwa ni wafanyabiashara wa Madini wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya ambapo watano (5) kati yao wamesomewa mashtaka tofauti ya uhujumu uchumi ikiwemo utoroshaji wa madini na wengine watano (5) wamewekwa chini ya uangalizi wa Mahakama kwa kipindi cha mwaka mmoja ili wawe na mwenendo mzuri.

 
Katika kesi ya kwanza ambayo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Andrew Scout inawahusu watuhumiwa watatu ambao ni Mike Konga, Sauli Solomon na Emmanuel Kessy ambao wamesomewa mashtaka matatu.

Akiwasomea mastaka yao Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe alisema shitaka la kwanza ambalo linawahusu watuhumiwa wote watatu ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Alisema kuwa kati ya Juni Mosi na Juni 30, mwaka huu watuhumiwa hao walijipatia fedha za Zambia kiasi cha Kwacha 290,000 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa raia mmoja wa Zambia kwa kumuuzia dhahabu kinyume na Sheria.

Aidha, Wakili Namkambe alisema kosa la pili la watuhumiwa hao ni utakatishaji wa fedha kiasi cha kwacha 290,000 ambazo walizipata kwa udanganyifu kutoka kwa raia wa Zambia.

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na Wakili Namkambe akadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena,  ambapo Hakimu Andrew Scoult aliihairisha kesi hiyo hadi Septemba 23 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamini hapo.

Katika kesi ya pili, mbele ya Hakimu Denis Luwongo, watuhumiwa wawili, Mike Konga na Sauli Solomoni wamesomewa mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha. 

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Basilius Namkambe ameiambia Mahakama kuwa watuhumiwa kwa pamoja kati ya Juni Mosi na Juni 30 mwaka huu walijipatia fedha kiasi cha dola za Marekani 115,000 kwa njia ya udanganyifu baada ya kumuuzia Henry Clever, raia wa Ujerumani madini aina ya dhahabu kilo moja kinyume na sheria. 

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. 

Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akawasilisha maombi ya kutaka baada ya kuhairishwa kwa kesi hiyo, Mtuhumiwa wa Pili, Sauli Solomon achukuliwe na Jeshi la Polisi kwa ajili ya upelelezi. 

Maombi hayo yalisababisha mvutano na wakili wa utetezi Baraka Bwilo ambaye alisema kuwa mteja wake alikamatwa tangu Septemba Mosi mwaka huu na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa mahojiano na muda wote huo alikuwa mikononi mwa Polisi, hivyo ni vema apelekwe gerezani na kama watamuhitaji kwa upelelezi wamfuate huko.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Namkambe alisema kuwa ombi lake ni sahihi kwa vile hata kama ni kumfuata huko ni lazima Mahakama itoe idhini hivyo ni busara aruhusiwe kwenda Polisi ili kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kuepuka malalamiko yanayoweza kujitokeza baadaye kuhusu upelelezi kuchelewa kukamilika.

Hakimu Denis Luwongo akatoa uamuzi wa kuruhusu mshtakiwa kuchukuliwa na Polisi kwa ajili ya upelelezi na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23, mwaka huu.

Kesi ya tatu ambayo imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Happiness Chuwa iliwahusu watuhumiwa wawili, Everine Bahati na Tyson Jeremiah ambao wamesomewa makosa matatu.

Wakili Basilius Namkambe aliiambia Mahakama kuwa katika kosa la kwanza watuhumiwa walikamatwa na madini aina ya dhahabu kiasi cha gramu 33.21 yenye thamani ya shilingi milioni 3 bila kuwa na kibali chochote.

Katika kosa la pili watuhumiwa wanadaiwa kujipatia fedha kwa udanganyifu kwa kuuza madini hayo bila kuwa na kibali huku wakijua kuwa ni kosa.

Wakili Namkambe alisema kuwa katika kosa la tatu ni utakatishaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 3 ambazo walijipatia kwa njia ya udanganyifu.

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na Hakimu Happiness Chuwa akaahirisha shauri hilo hadi Septemba 23, mwaka huu litakapotajwa tena mahakamani hapo.

Katika kesi nyingine wafanyabiashara watano wa madini wamepandishwa kizimbani chini ya kiapo cha faragha kilichosainiwa na Mkuu wa upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ambapo Serikali imeomba watu hao wawekwe chini ya uangalizi maalum ili wawe na mwenendo mzuri.

Wakili Namkambe amesema ombi hilo linatokana na watuhumiwa kufanya makosa mengi ya mara kwa mara.

Baada ya kusomwa kwa maombi hayo, watuhumiwa wote hawakuwa na pingamizi na badala yake wakaomba walegezewe masharti ya dhamana na ndipo Hakimu akawaweka chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 12 ambapo watatakiwa kuripoti kwa wakuu wa Polisi wa Wilaya mara moja kila mwezi.

Hata hivyo ,watuhumiwa hao walitakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya shilingi milioni 10 ili wapewe dhamana.

Watuhumiwa wawili pekee ndio waliotimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru na watatu wamerejeshwa rumande hadi Ijumaa ya Septemba 13, kesi hiyo itakapotajwa tena na wao wametakiwa kufika na wadhamini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa madini Stanslaus Nyongo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuachana na biashara haramu za madini na badala yake wafanyebiashara hiyo kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu ikiwemo kufilisiwa mali zao na kwenda jela.

Mashataka hayo yalisomwa Septemba 9, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527