KUELEKEA MTIHANI WA TAIFA 2019, RC MTAKA AWAFUNDA DARASA LA SABA SIMIYU

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Kuelekea katika Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu elimu ya Msingi Darasa la saba Septemba 11-12, 2019 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewaonya wanafunzi wa darasa la saba mkoani hapa kujiepusha na udanganyifu katika mtihani huo badala yake wazingatie waliyofundishwa na kufanya mtihani huo kwa utulivu na kujiamini.

Mtaka ameyasema hayo Septemba 09, 2019 wakati akizungumza na wanafunzi wa darasa la saba kutoka katika Kata ya Lamadi wilayani Busega Septemba 09, 2019 katika Shule ya Msingi Mwabasabi, kwa niaba ya wenzao wa Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwatakia heri katika  mtihani wa Taifa wanaotarajia kuufanya kuanzia Septemba 11-12, 2019.

Mtaka amesema anaamini walimu wamefanya kazi yao vizuri ya kuwafundisha na kuwaandaa wanafunzi  hao hivyo ni vema wakafanya mtihani huo wakiwa na ujasiri huku wakipuuza taarifa zozote za kuwepo kwa majibu ya mitihani mahali popote.

“Ninawatakia kila la heri kwenye mtihani wenu, nashukuru kwa kazi nzuri iliyofanywa na walimu katika kuwafundisha na kuwaandaa kwa kutoa majaribio ya mara kwa mara, kambi kambi za kitaaluma; niwaombe mkaufanye mtihani huu kwa utulivu na ujasiri; asiwadanganye mtu kuwa kuna majibu ya mtihani au mtihani umevuja sehemu fuulani, mkazingatie mlichofundishwa” alisema Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka amewashukuru walimu kwa namna wanavyojituma katika kuwafundisha wanafunzi na kutoa wito kwa walimu hao kuanzisha madarasa ya maandalizi ya kidato cha kwanza (pre- form one)  kwa wanafunzi hao wanaohitimu ili wasaidie kuwaandaa wanafunzi hao na  masomo ya kidato cha kwanza na waweze kupata kipato cha ziada kupitia malipo yatakayotolewa na wazazi watakaokuwa tayari kugharamia masomo hayo.

Kwa upande wake Afisa Taaluma Mkoa wa Simiyu , Mwl. Onesmo Simime amesema Mkoa wa Simiyu uliweka mikakati mbalimbali ya maandalizi ya wanafunzi wa darasa la saba ikiwemo walimu kumaliza mada zote mwezi Juni 2019 na kuwepo kwa kambi za kitaaluma kwa kila shule,  hivyo wanafunzi wameandaliwa vizuri na kwa mikakati hiyo matarajio ya mkoa ni ufaulu kuongezeka zaidi ya mwaka jana 2018.

Akizungumza kwa niaba ya walimu, Mwalimu Beatrice Ernest kutoka Shule ya Msingi Mwabasabi amesema wana uhakika na maandalizi waliyofanya kwa wanafunzi wao hivyo  ufaulu utaongezeka, huku akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwaruhusu kuanzisha vituo vya ‘pre-form one’ na kuahidi kuwa walimu watajiunga kuanzisha madarasa hayo ili kuboresha taaluma ya wanafunzi wao na kuboresha vipato vyao.

Nao baadhi ya wanafunzi wakizungumza kwa niaba ya wenzao wamesema wamejiandaa vizuri na wamejipanga  kufanya vizuri ili waweze kutimiza malengo yao ikiwa ni pamoja na  kujiunga na elimu ya sekondari na hatimaye kuendelea na elimu juu ili waweze kufikia ndoto zao.

“Mimi na wenzangu wote tumejiandaa vizuri nina uhakika tutafanya vizuri na wote tutaenda sekondari, ushauri tuliopewa na Mkuu wa Mkoa tutauzingatia naamini tutashinda tu” Eric Malimi kutoka Shule ya Msingi Lamadi.

“Sisi tumejiandaa vizuri na tunaweza kuendelea mbali kimasomo, tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutupa mawaidha na tutayatekeleza ili tuweze kufaulu mtihani wa Taifa na tufikie tunapotaka” alisema  Glorymary Samwel kutoka Shule ya Msingi Itongo.

Mkoa wa Simiyu una jumla ya wanafunzi 29,248  wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa Septemba 11-12, mwaka huu, ambao kati yao  wavulana ni  13, 594 na wasichana 15.654.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527