SERIKALI YAWATAKA WADAU WA KILIMO WAWASILIANE NA BENKI YA TADB KUPATA MIKOPO

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Serikali imetoa wito kwa wadau wote wa kilimo nchini kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo –TADB ili waweze kupata maelekezo sahihi ya uandaaji wa miradi itakayokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na benki hiyo.

Wito huo umetolewa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Mbeya Vijijini , Mhe. Oran Njeza, aliyetaka kujua mkakati wa Benki ya Kilimo kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, Benki ya TADB imefikisha huduma zake mkoani Mbeya na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka Sh. milioni 799.9 mwezi Desemba 2017 hadi Sh. bilioni 2.54 kufikia Aprili, 2019.

Alisema kuwa mikopo imetolewa kwa miradi 7 ya kilimo na kuwanufaisha wakulima 509 wa Nyanda za Juu Kusini katika wilaya za Mbozi, Momba na Mbalali.

“Benki ya TADB imefanikiwa kufungua Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoani Mbeya, lengo likiwa kuhakikisha Benki hiyo inasogeza huduma zake karibu zaidi na wateja ambao ni wakulima wote wa Nyanda za Juu Kusini, ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya Vijijini”, alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa Benki ya TADB inakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima, Serikali imeipatia benki hiyo kiasi cha Sh. bilioni 103, kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB.

Aidha kwa sasa Benki hiyo inaendelea na mchakato wa kukamilisha masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa Sh. Bilioni 103 kutoka Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika.

Benki ya TADB tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2015, TADB imefanikiwa kujiendesha na kukuza mtaji wake hadi kufikia Sh. Bilioni 67.5 zilizo rekodiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2019 kutoka Sh. Bilioni 60 mwezi Novemba, 2014.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527