MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AZUNGUMZIA DALILI YA 'MLIPUKO WA VOLCANO' NDEMBEZI



Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack, ametoa tahadhari kwa wananchi wa eneo la Ndembezi Mazinge Manispaa ya Shinyanga kutokana na uwepo wa dalili za Volcano.
Akiongea na EATV & EA Radio leoTelack, amesema kuwa amewataka wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, kukaa mbali ili kuepuka kupata madhara endapo hali hiyo ikiwa sio ya kawaida.

'Hili eneo linaonekana kama lava au Volcano, lakini hatujathibitisha bado maana udongo unaotoka ni wa baridi, sasa isije kutokea udondo wa moto ukaleta madhara', ameeleza.

Aidha mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa, 'Hili suala lipo kwa wiki ya pili sasa na ni karibu kiasi na makazi ya watu lakini Watalaamu wa Jiolojia walikuja na hawakubaini madhara yoyote lakini leo (Septemba 21, 2019), kuna watalaamu wanaingia wao ndio watatueleza zaidi'.

Kuhusu mazingira ya eneo, RC Telack amesema kuwa ni kilima ambacho sio kikubwa sana lakini kimekuwa kikitoa udongo tepetepe, ambao unatoka chini kupanda juu lakini kwa mujibu wa wazee wa zamani katika eneo hilo, hicho kitu si cha kawaida kihistoria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527