NAIBU SPIKA DKT TULIA : UAMUZI WA SERIKALI KUBORESHA MIUNDO MBINU IMESAIDIA KUKUZA UTALII KUSINI


Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dkt.  Tulia Ackson akisalimiana na mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo leo katika maonesho ya utalii ya Karibu Kusini 
Mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa akisalimiana na Naibu Spika Dkt.  Tulia Ackson leo 
Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Joseph Ryata akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dkt Tulia Ackson leo 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ali Hapi akitoa salam za mkoa wakati wa maonesho hayo ya utalii leo
**
Na Francis Godwin - Iringa

NAIBU Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema uamuzi wa serikali ya awamu ya tano wa kuboresha miundo mbinu ya viwanja vya ndege katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini utasaidia kuvutia watalii katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Dkt.  Tulia aliyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya kitalii ya kimataifa ya Karibu Kusini  yanayoendelea katika viwanja vya Kihesa Kilolo mjini Iringa, ambapo ameeleza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt.  John Magufuli imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya utalii nchini ambalo linaendelea kuliongezea taifa fedha za kigeni.

Alisema  ni muhimu sana kwa Watanzania wote kushiriki kukuza utalii kwa kutembelea hifadhi za utalii ili kukuza sekta ya utalii nchini kwani sekta ya utalii inachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi.

"Ndugu zangu nimeeleza namna gani sisi wenyewe tunavyoweza kushiriki katika kutembelea hivi vivutio lakini pamoja na hayo nitoe wito ambao tunatakiwa sisi sote kuwa wazalendo wa kutangaza utalii wetu nyanda za juu kusini na nashukuru leo vyombo vya habari vipo kwa wingi leo hapo hivyo tunatamani kuona taarifa hizi zinasambaa zaidi maana kalamu zenu zinafika mbali zaidi" ,alisema Dkt Tulia.

"Pia niungane na mbunge Peter Msigwa kuwa lazima sisi wenyewe tuwe sehemu ya ubunifu wa kuvutia watalii waweze kufika kutembelea vivutio hivyo kwa kuwa na vitu tofauti vya kuwafanya watalii kuweza kufika kutembelea vivutio vya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini",alisema.

Dkt Tulia alitaka wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na viongozi kuwa wabunifu wa kubuni vitu vya kuvutia watalii kuja kutalii kwenye hifadhi za mikoa ya nyanda za juu kusini kwani bila kuwa wabunifu wa vitu tofauti nje ya vile vilivyozoeleka basi itakuwa ngumu kuwafanya kuja kutalii katika mikoa ya kusini.

Alisema wapo baadhi ya watalii ambao kwao kuona mimea ya mazao mbalimbali kama mahindi na mimea mingine kwao ni utalii ambao sehemu nyingine hawaoni hivyo wakija huku kusini wataweza kujifunza zaidi.

Dkt. Ackson alisema Mikoa ya Kusini kuna vivutio vingi ambavyo watalii wanaweza kuja kujifunza hivyo kazi kubwa iwe ya kutangaza vivutio hivyo vya utalii na kama kuna vitu bidhaa ambazo zinasindikwa mikoa ya nyanda za juu kusini kama maziwa na majani ya chai lazima kuanza nayo kuyataganza ili watalii wakifika kujivunia bidhaa hizo kutoka Iringa.

Alieleza  kuwa suala la gereza la Kihesa Mgagao lililopo wilaya ya Kilolo kuwa sehemu ya utalii kutokana na historia yake ya kuwa ni sehemu ya kudai uhuru wa nchi za kusi mwa Afrika .

Awali mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi akimkaribisha mgeni huyo rasmi Dkt. Tulia kufungua monyesho hayo alisema kuwa mikoa ya Nyanda za  Juu Kusini imejipanga kutangaza utalii wa mikoa hiyo na kuwa kupitia maonesho hayo ya karibu kusini wanategemea sekta ya utalii itaendelea kukua zaidi 

Akizungumza katika maonesho hayo mtendaji mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kuhusiana na jitihada zinazofanywa na serikali katika kutatua changamoto za utalii nyanda nyanda za juu kusini hasa katika miundo mbinu alisema kuwa serikali mchakato wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha unaendelea na upo hatua nzuri na fedha zake zimeopatikana kutoka benki ya dunia na wakati wowote ujenzi wake utaanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527