DC MWAIMU AWATANGAZIA KIAMA WANAOHUJUMU MIRADI YA MAENDELEO KYERWA


Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Mh. Rashid Mwaimu

Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera Mhe. Rashid Mwaimu 
amesema atapambana vikali usiku na mchana ili kuhakikisha anakomesha watu wanaotaka kuhujumu miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi itolewayo na serikali akibainisha kuwa yupo tayari kukesha katika maeneo yote ya miradi ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya hiyo Rashid Mwaimu ametoa kauli hiyo Septemba 27.2019 ofisini kwake wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo wilayani hapo.

Mhe.Rashid amesema atahakikisha analinda na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoletwa na serikali wilayani humo huku akiahidi kuwashughulikilia wale wanaotaka kufanya vitendo vya kuihujumu serikali.


Amesema kutokana na jitihada, nguvu na busara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika utekelezaji wa miradi ya ki maendeleo yeye kama mkuu wa wilaya hatomfumbia macho mtu yeyote anayepanga kuhujumu miradi hiyo.


"Nawaahidi miradi yote inayoletwa na serikali kwa ajili ya wilaya ya Kyerwa nitaisimamia na kuilinda kwa nguvu zote, nitahakikisha adui yeyote haisogelei miradi hiyo ,miradi ni mali ya wananchi ole wenu mliozoea kuitafuna muda umekwisha, nitacheza na nyie usiku kucha", alisema Mwaimu.

Hata hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuwahimiza kutomchagua kiongozi mbishi, badala yake wachague kiongozi ambaye ni mzalendo na muadilifu atakayewaletea maendeleo.

Katika suala la ulinzi na usalama, amesema katika wilaya yake ulinzi na usalama ni wa kutosha hivyo amewataka wananchi kuripoti katika vyombo husika mara moja vinapojitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani kwa baadhi ya watu wasiowaadilifu hasa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527