TANZANIA YAITOA BURUNDI KWA MATUTA NA KUSONGA MBELE KUFUZU KOMBE LA DUNIA QATAR 2022


Na Saada Salim, Dar es salaam
Tanzania imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kwa ushindi wa penalti 3-0 kufuatia sare ya 1-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Sare ya 1-1 yalikuwa marudio ya matokeo ya mchezo wa kwanza Uwanja wa Intwari mjini Bujumbura na kufanya sare ya jumla ya 2-2 kabla ya kipa mzoefu, Juma Kaseja Juma kwenda kuibuka shujaa kwenye mikwaju ya penalti.

Beki mkongwe anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni alianzisha biashara nzuri kwa Taifa Stars baada ya kufunga penalti ya kwanza na wenzake, kiungo Himid Mao Mkami ‘Ninja’ na beki Gardiel Michael Mbaga wakafunga pia.

Kaseja aliwakata maini Warundi baada ya kuokoa penalti ya kwanza ya Int’hamba Murugamba iliyopigwa na mtokea benchi, Omar Ngandu aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kanakimana Bienvenu Kanakimana dakika ya 67 na haikuwa ajabu Saido Berahino na Bigirmana Gael wakapiga nje mfululizo. 

Katika dakika 90 za mchezo, Nahodha na mshambuliaji Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aliitanguliza Taifa Stars kwa bao lake la dakika ya 30 akimalizia kona ya beki wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy anayechezea Nkana FC ya Zambia.

Mpachika mabao anayeondoka JS Kabylie ya Algeria kuhamia Ligi Kuu ya Misri, akaisawazishia Burundi dakika ya 45 akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji chipukizi, Amissi Mohammed anayechezea timu ya vijana ya NAC Breda ya Uholanzi.

Walinzi wa Taifa Stars, Nyoni na Kelvin Patrick Yondan leo kwa mara nyingine walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji wa Zulte-Waregem ya Ubelgiji, Berahino ambaye siku yake ikaisha vibaya zaidi baada ya kukosa penalti pia.

Taifa Stars inaungana na washindi wengine 13 wa hatua ya mchujo kuungana na timu nyingine 26 za viwango vya juu barani, wakiwemo majirani Kenya na Uganda kuingia kwenye makundi 10 kuanza rasmi kuwania tiketi ya Qatar 2022.

Washindi 10 wa kwanza wa makundi yote watamenyana baina yao katika hatua ya tatu na ya mwisho mchujo wa mbio hizo za Qatar na timu tano zitakazoshinda ndizo zitaiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia lijalo.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa: Juma Kaseja, Hamis Ramadhani, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Gardiel Michael dk70, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Idd Seleman, Abubakar Salum ‘Sure Boy’/Shaaban Chilunda dk72, Mbwana Samatta/Himid Mao dk106, Saimon Msuva na Hassan Dilunga/Farid Mussa dk60.

Burundi: Ndikumana Justin/Nahimana Jonathan dk119, Diamant Ramazani, Racanamwo Joel, Nsabiyumva Fredric/Nahimana Shassiri dk85, Nshihirimana David, Bigirmana Gael, Amissi Cedric, Kanakimana Bienvenu/Omar Ngandu dk67, Berahino Saido, Abdul Fiston/Bimeyimana Bin-Flies Caleb dk70 na Amissi Mohammed.

Via>Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post