POLISI PWANI YAKAMATA MADUMU 859 YA MAFUTA YA KULA YASIOLIPIWA USHURU TAKRIBAN MIL.50


NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
JESHI la polisi mkoani Pwani, limekamata madumu 859 ya mafuta ya kula yanayodaiwa kutolipiwa ushuru ,yenye thamani takriban milioni 50 ,huko Chemchem kata ya Magomeni ,Bagamoyo.


Akithibitisha kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani hapo,Wankyo Nyigesa alisema ,madumu hayo yalikuwa yakisafirishwa na Christopher Emmanuel (32).


Alieleza kuwa, Christopher aliyasafirisha madumu hayo kupitia gari yake namba T.621 BCG aina ya fuso baada ya kukwepa kulipa ushuru kwenye moja ya bandari bubu Bagamoyo.


“Tunachunguza risiti zake za malipo kwani pia zina TIN namba tofauti,tunamshikilia mtu huyu pamoja na aliyeshirikiana nae kutoa Hassan Saidi mpemba huyu mkazi wa Bagamoyo.”


Wankyo alisema, huo ni usafirishaji haramu na kulitia hasara Taifa kwa kukwepa kulipa ushuru ama kodi,hivyo aliwaasa wananchi kuacha biashara za magendo.


Kamanda huyo alifafanua, wafanyabiashara wanapaswa kulipa ushuru kwa maendeleo ya Taifa na sio kutaka faida kwa njia za mkato.


Alibainisha hawatawaachia nafasi wakwepa ushuru na kudhibiti mianya ya kukwepa ushuru kwenye bandari zote bubu kwakuwa zinafahamika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527