SERIKALI YAAGIZA MADUKA YA PEMBEJEO ZA KILIMO YAKAGULIWE SHINYANGA


Mkuu wa mkoa wa Shinyang Mhe. Zainab Telack

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Serikali Mkoani Shinyanga imeagiza kufanyika kwa ukaguzi wa maduka yote pembejeo za kilimo mkoani humo baada ya kubainika kuwepo kwa yanayouza dawa na pembejeo ambazo hazina ubora kabla ya msimu wa kilimo ambao unataraji kuanza hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na maendeleo ya mkoa wa Shinyanga (RCC),ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo Zainab Telack  ambapo amesema Maafisa (TFDA) na (TBS) wanapaswa kufanya kazi hiyo kwa haraka ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo bora.

Amesema baadhi ya wamiliki wa maduka ya pembejeo mkoani humo wamebainika kuuza pembejeo zisizokizi viwango kama vile mbegu na dawa ambazo zimeshakwisha muda wake na kusababisha wakulima kupata hasara kwa kutoota pindi wanapopanda.

Telack amefafanua kuwa endapo hatua za haraka zisipochukuliwa kwa wamiliki hao wataendelea kujinufaisha wao wenyewe na kuisababisha malalamiko kutoka kwa wakulima hivyo mamla husika zinatakiwa kuwa makini.

Sanjari na hilo Telack amesema kuna baadhi ya maduka yapo katika mkoa wa shinyanga na hayana usajili kutoka mamlaka husika na wanaendelea kutoa huduma jambo ambalo ni kinyume na sheria na wanaweza kuhatarisha usalama wa wakulima pindi wanapowapa huduma.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad ameshauri ukaguzi huo uwe ni endelevu na TFDA na TBS ni lazima wahakikishe watumishi wanaouza maduka hayo wawe na sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa leseni zao.

Ameongeza kuwa wapo baadhi ya wamiliki wa maduka hayo wamekuwa wakiwapa watu wasio kuwa na sifa kuuza maduka ya pembejeo hali ambayo inaweza kusababisha wakulima wakapata hasara kutokana na kutokuwepo kwa umaki katika utoaji huduma.

Amefafanua kuwa katika mkoa wa shinyanga baadhi ya mifugo imebainika kupewa chanjo ambazo hazina ubora na kusababisha mifugo kufa na mbegu kutoota jambo ambalo lisipochukuliwa hatua za haraka linaweza kuleta madhara kwenye jamii.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza
Wadau wakiwa ukumbini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527