
Na Annastazia Paul - Malunde 1 blog
Wazazi na walezi katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea chanjo kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya Surua-rubella na polio itakayoanza kutolewa Septemba 26 hadi Septemba 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Manispaa Dk. Charles Malogi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, ambapo amesema kuwa chanjo hiyo itatolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 9 hadi 59.
"Kinga pekee ya magonjwa haya ni chanjo na hayana tiba ya moja kwa moja hivyo ikitokea mtu amepatwa na magonjwa haya huwa tunatibu zile dalili zake, kama vile homa kali, mafua na kikohozi",amesema Dk. Malogi.
Kwa upande wake mratibu wa chanjo wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Dk. Sanya Mwara amesema kampeni hiyo ya chanjo ni ya kitaifa na kwamba itafanyika kwa muda wa siku tano kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi 12:00 jioni.
"Tunatarajia kutoa chanjo ya surua-rubella kwa jumla ya watoto 22,984, na watoto 14,346 watapatiwa chanjo ya polio katika Manispaa ya Shinyanga",amesema Dk. Mwara.
Amesema kuwa chanjo hizo ni muhimu na hazina madhara yoyote kiafya hivyo kuwataka wananchi wote kuwapeleka watoto wao katika vituo hivyo vya kutolea chanjo, na kwamba chanjo hizo zimethibitishwa na shirika la afya Duniani WHO na Wizara ya afya.
Naye afisa chanjo msaidizi wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dk. Ram Haji Ram amesema kuwa chanjo hiyo imekuwa ikitolewa kila baada ya miaka mitano kutokana na utolewaji mdogo wa chanjo hizo katika nchi jirani.
"Tanzania tunapakana na nchi nyingi ambazo utoaji wake wa chanjo za magonjwa hayo ni mdogo, pia kuna muingiliano wa watu katika nchi hizi jirani hivyo kuna uwezekano wa maambukizi ya magonjwa hayo kutoka nchi jirani ikizingatiwa kuwa huambukizwa kwa njia ya hewa, ndiyo maana hapa nchini chanjo za magonjwa hayo hutolewa kila baada ya miaka mitano",amesema Dk. Ram.
Social Plugin