ABIRIA 56 WANUSURIKA KIFO BAADA YA BOTI KUWAKA MOTO KATIKA ZIWA VICTORIA

Watu 56 nchini Tanzania wamenusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria katika ziwa Victoria mkoani Kagera kuwaka moto.

Boti hiyo ilikuwa ikitoka Kemondo kuelekea Bumbile ziwani.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi ameviambia vyombo vya habari kuwa boti hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 84 lilikuwa na abiria 56 pamoja na mizigo.

"Safari ya boti hiyo inayofahamika kama Mv Lulimbe ilianza majira ya saa nane na nusu mchana Septemba 16, 2019 , lakini iligeuza kurudi bandarini baada ya muda mfupi baada ya kuona moto umeanza kushika.

Baada ya kutokea itilafu hiyo, injini ilizima na kuleta tafrani iliyosababisha wengine kujitosa majini na kuokolewa.

Majeruhi ni watatu ambao wote ni wanawake, kwa sasa wamelazwa lakini daktari anasema wanaendelea vizuri.

Uchunguzi bado unaendelea kwa sababu hatujui chanzo cha ajali hii licha ya ingini kuzima"Kamanda alieleza.

Michael Dominick, mkazi wa Isamilo ni miongoni mwa abiria walioshuhudia boti hiyo, Yeye anasema kuwa boti ilianza kuwaka moto muda mfupi baada ya kuondoka bandarini, "Ulitokea mlipuko eneo la nyuma ya boti katika injini na kusababisha moto mkubwa".

"Abiria walipiga kelele kuomba msaada na wengine waliruka katika maji na kuogelea ila bado sijawaona wawili kati yetu ambao ni mwanamke na mwanaume,"Dominick ambaye ni mvuvi pia alisimulia hali ilivyokuwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewapa pole wananchi hao, kuwataka kuhakikisha wanazingatia usalama wao wakati wa kusafiri sambamba na wakaguzi wa vyombo vya majini kufanya ukaguzi.

"Wananchi mtusaidie Serikali kwa kuhakikisha mnavikagua vyombo hivi kabla ya safari mkivitilia mashaka toeni taarifa kwa mamlaka husika ili tuweze kudhibiti ajali hizi kabla ya kutokea," amesema mkuu huyo wa Mkoa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527