MGEJA AMSHAURI MEMBE AFUATE NYAYO ZA LOWASSA


Khamis Mgeja

Na Paul Kayanda-Kahama

MWENYEKITI wa taasisi yaTanzania Mzalendo Foundation Khamis Mgeja amemshauri aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya nne Benard Membe afuate nyayo za Waziri mkuu mstaafu Mhe. Eduard Ngoyai Lowassa kuiga mfano wake wa kuwa na ustaarabu na uungwana wa kisiasa na akubali yaishe.

Mgeja aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kijijini kwake Nyanhembe Kata ya Kilago Halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga ambapo alizungumzia kauli tata za mara kwa mara za mwanachama wa CCM Benard Membe alizozitoa hivi karibuni na kudai kuwa kauli hizo zimekosa uadilifu ndani ya chama na serikali pamoja na utu na heshima kwa mtu aliyejaa imani za dini.

Mwenyekiti huyo wa taasisi hiyo inayoshughulika na masuala ya haki, Demokrasia na Utawala Bora, amesema amekuwa akimfuatilia mara kwa mara kauli zake anazozitoa kupitia vyombo vya Habari pamoja na mitandao ya kijamii Twitter.

Mgeja alisema kuwa Membe amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kupata hadhi ya kuwa mwanadiplomasia lakini kauli anazozitoa hazilingani na hadhi yake kama mwanadiplomasia wala mtu aliyeishi na imani ya dini utu na uungwana.

“Mfano wanadiplomasia kama Membe wote Duniani hupenda kufanya kazi za kupigania maridhiano na mapatanisho na pale wanapokoseana huwahi kuombana radhi inasikitisha kuona matendo na kauli anazoto marakwa mara Membe inawezekana kabisa hakuiva vizuri katika masuala ya Diplomasia,” alisema mwenyekiti wa Mzalendo Foundation Khamis Mgeja huku alitolea mfano.

Aidha Mgeja alisema, Membe kama mwanachama hai wa CCM hakustahili kabisa kutoa maneno hayo labda awe rangi mbili aliyejificha kwa kimvuli cha CCM na kauli hizo zinamvunjia heshima na uadilifu mbele ya chama chake na kumuondolea hadhi na heshima ya mwanadiplomasia na kugeuka hivi sasa kuwa mwanaharakati.

“Nimkumbushe Membe kuwa CCM hivi sasa inavyoonekana ni kwa vitendo iko imara sana kama ilivyokuwa siku za nyuma enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wote tumeona mageuzi makubwa CCM iliyoyafanya ndani ya chama chini ya mwenyekiti wa Taifa Dk. John Pombe Magufuli na sekretelieti nzima ikiongozwa na katibu mkuu Dk. Bashiru Ali ndiyo maana mimi Mgeja na Mheshimiwa Lowassa na wengine tuliamua kurudi CCM ili kuja kushirikiana kwa pamoja tukiwa ndani ya CCM kujenga nchi yetu kwa maendeleo ya Taifa, na tulikubali yaishe,”alisema Mgeja.

Mgeja alimfahamisha Membe kuwa uimara wa chama ni kuona serikali yake ya awamu ya tano inavyotekeleza ilani kwa weledi na kwa kiwango cha hali ya juu sana katika miradi mikubwa inayotekelezwa hivi sasa hasa katika upande wa sekta mbalimbali za miundo mbinu, Reli, Ndege, barabara, usafiri majini uboreshwaji wa huduma za jamii kama afya elimu, umeme maji kilimo, uvuvi, ufugaji, sekta ya mali asili na utalii, sekta ya Madini, viwanda pamoja na kupiga vita ubadhilifu wa mali za umma.

Pamoja na mambo mengine Mgeja alisema kuwa kwa uzoefu wake katika masuala ya kisiasa anavyomuona Membe njia anayoenda nayo na kupitia katika harakati zake za kisiasa zilizojificha haziwezi kumfikisha popote pale kwa kujitafutia umaarufu wa siasa nyepesi ni vyema asome alama za nyakati na atambue kila zama na kitabu chake, watanzania wa leo hawadanganyiki na kwamba anampa ushauri wa bure akatafute kazi nyingine ya kufanya hata kilimo kitamsaidia.

Mgeja alisisisitiza katika ushauri wa bure kwa Membe ana wajibu kama mwana CCM na wenzake waliojificha nyuma yake ni vyema na busara wakubali yaishe tu na wapate muda mrefu wa kuzungumzia kwa wananchi mafanikio yote mazuri yanayofanywa na serikali ya CCM ya awamu ya tano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527