MBWA KICHAA ALIYEJERUHI WATU 18 NDANI YA SIKU 2 BUKOBA AUAWA


Mbwa aliyejeruhi watu 18 akiwa ameuawa

Na Lydia Lugakila -Malunde 1 blog Bukoba
Wananchi katika kata ya Katoro Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wamefanikiwa kumuua mbwa tishio aliyekuwa na kichaa na kusababisha kuwajeruhi kwa kuwang’ata wananchi 18  katika kata hiyo.

Akizungumza na Malunde1 blog leo Septemba 8, 2019,
Afisa mtendaji wa kata ya Katoro Innocent Mzungu ambaye ameeleza kuwa mbwa huyo amekuwa tishio kwa kuwang’ata wananchi 18 na kusababisha watoto na watu wazima kujifungia ndani na wanafunzi kushindwa kwenda shule kutokana na hofu ya kushambuliwa na mbwa huyo.

Ameeleza kuwa mbwa huyo alifanya madhara kwa wananchi kati ya Septemba 5 na 6 mwaka huu kwa kujeruhi wananchi 18.

Amesema kutokana na tukio hilo wananchi wa kijiji cha Ruhoko wamefanikiwa kumuua mbwa huyo na kutolewa tamko kwa kila mwananchi aliyefuga mbwa na paka kuwapeleka wanyama hao kupatiwa chanjo Septemba 9 mwaka huu na watakaokiuka watatozwa faini.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Mhe. Hashimu Murshid Ngeze amesema mwezi uliopita baadhi ya wananchi wa kata ya Rukoma waliwang’atwa na mbwa mwenye kichaa jambo lililowafanya viongozi wa halmashauri ikiwemo idara ya mifugo kukubaliana kwa pamoja kuwa mbwa ambao wanabainika kuwa na kichaa wachanjwe kwani hivi karibuni dawa za kuchanja zililetwa na tayari zoezi la kuwapa chanjo mbwa hao linaendelea ndani ya wilaya hiyo.

"Mwaka 2018 mbwa baadhi walichanjwa lakini wananchi akiwemo wafugaji wenyewe walikaidi kupeleka mifugo hiyo kupata chanjo natoa agizo kila mbwa achanjwe.Natoa wito kwa wananchi wanaofuga mbwa kuhakikisha wale ambao wanasadikika kuwa na kichaa wafungiwe ndani wakati zoezi la kuwachanja likiendelea",amesema.

Aidha amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wanashirikiana na wananchi ili kufanikisha zoezi hilo na kuwa ni agizo la lazima kila mbwa kupatiwa chanjo ili kuepusha madhara katika jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527