ONGEZEKO LA NYUMBA ZA KUABUDIA LACHANGIA KUPUNGUA KWA MAUAJI YA VIKONGWE NA WATU WENYE UALBINO SHINYANGA

Msikiti wa Masijd Al Ikhilas Mbulu uliofunguliwa Kahama
Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Kuongezeka kwa maeneo ya kuabudia hususani Misikiti wilayani Kahama mkoani Shinyanga kumetajwa kupunguza jamii kutenda vitendo vya ukatili kama vile mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino kutokana na watu kuwa na hofu ya Mungu.


Hayo yamebainishwa leo na Sheikh wa wilaya ya Kahama Alhaj Omari Damka kwenye hafla maalumu ya Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa Masijd Al Ikhilas Mbulu uliopo katika Mtaa wa Mbulu katika Halmashauri ya Mji wa Kahama.

Amesema kwa sasa mauaji hayo yamepungua kutokana na jamii kuachana na vitendo vya ukatili vilivyokuwa vikichangiwa na imani potofu kuhusiana na wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi katika mkoa wa shinyanga.

Sheikh Damka amesema viongozi wa dini wanajukumu kubwa la kuibadilisha jamii kwa kuhakikisha inakuwa na amani na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali ambazo zitawasidia kupata vipato halali katika familia zao.

“Jamii inapaswa kuacha dhana hiyo potofu na badala yake wadumishe amani ikiwa ni pamoja na kuunga mkono shughuli zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Dk John Pombe Magufuli kwa kwenda kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linaendelea wilayani humo”,alisema Sheikh Damka.

Naye Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiislamu ya International Istiqaama Community, Sheikhe Ahmed Mohamed Alhapsy amewataka waumini wilayani humo kuacha kubaguana na badala yake washirikiane katika kuijenga jamii ili iendelee kuwa na amani.

“Endapo Waislam wakianza kubaguana na kutoshirikiana kwa kigezo cha Madhehebu inaweza kukwamisha maendeleo ya dini sambamba kutofikisha ujumbe sahihi ambao wanapaswa kuutoa kwa waumuni wao”,alisema Ahmed.

Msikiti huo umejengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya Kiislamu ya International Istiqaama Community,chini ya Sheikh, Ahmed Haroun Alnooby.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527