CCM MISENYI KUNUNUA KIFAA CHA KUSAGIA CHAKULA KUSAIDIA MTOTO PACHA ALIYETENGANISHWA NA MWENZAKE

Lydia Lugakila- Malunde 1 blog
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilayani Misenyi mkoani Kagera wameahidi kununua (Brenda) kifaa cha kusagia chakula cha mtoto pacha Merrynes Benatus mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 8 aliyetenganishwa na mwenzake Anisia Benatus aliyefariki dunia wakati akitoka kwenye Matibabu nchini Saudi Arabia.

Viongozi hao wametoa ahadi hiyo leo Septemba 22, 2019 wakati wakiwa katika kituo cha Afya cha St. Therese kilichopo katika kata ya Mushasha wilayani Misenyi Mkoani Kagera wakati wakimjulia hali mtoto huyo anayeendelea na matibabu katika kituo hicho.

Awali Mama wa mtoto huyo Bi Jonesia Jovitus amesema licha ya hali ya mtoto Merrynes kuendelea kuimarika kutokana na juhudi za wahudumu wa kituo hicho kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali ya Muhimbili pamoja na Saudi Arabia lakini changamoto kubwa ni kifaa cha kusagia chakula cha mtoto huyo ambapo mama huyo amewaambia viongozi hao kuwa amekuwa akitwanga chakula hicho kutokana na ukosefu wa kifaa hicho.

Kufuatia hali hiyo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Misenyi mkoani Hassan Moshi ameahidi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu kukamilisha upatikanaji wa kifaa hicho ili mtoto huyo aweze kupata chakula chenye kiwango inayokubalika.

"Hiyo kazi sisi kama chama tutaifanya CCM kazi yake sio kutafuta kura jukumu letu pia ni kushiriki katika shida na raha za wananchi kwa ujumla, kwa hiyo mimi naahidi tutanunua Brenda hiyo na tungejua tungekuja nayo tulishindwa kujua tuje na nini kutokana na masharti ya mahitaji ya mtoto huyu",alisema.

Akitaja vyakula anavyovitumia mtoto Merrynes,   mama mzazi wa mtoto huyo amesema ni pamoja na wali uliosagwa nyama ya kuku wa kienyeji ,karoti vilivyosagwa na kwamba  haruhusiwi kutumia chumvi , sukari wala mafuta ya kula.

Mama huyo amewashukuru viongozi hao kwa kujitolea kununua kifaa hicho kwani amekuwa akipata adha kubwa katika kutengeneza na kuandaa chakula cha mwanae tangu awepo katika kituo hicho huku akiiomba serikali pamoja na jamii kwa ujumla kumsaidia kuboresha nyumba yake kwa kumuwekea umeme na kuiwekea sakafu nyumba hiyo , ili mtoto huyo aendelee kukua vizuri kwa kupata mwanga na kuwa katika nyumba isiyokuwa na vumbi.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho Francisca Francis, amewashukuru viongozi hao wa CCM huku akifurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo wa kumhudumia mtoto huyo kati ya madaktari kutoka Saudi Arabia na hospitali ya taifa ya Mhimbili wanaohakikisha mtoto huyo anaendelea vizuri kiafya.

Muuguzi mwangalizi wa mtoto huyo Dina Kajuna amesema wanaendelea kufuata masharti ya wataalam wa afya kutoka ndani na nje ya nchi na kufurahishwa na wadau mbalimbali wanaofika kituoni hapo kumfariji mama na mtoto huyo.

Aidha Bi Kajuna amewapongeza viongozi wa chama cha mapinduzi ccm wilayani Wilayani Misenyi na ametoa wito kwa jamii kuachana na suala la kupenda kuchangia sherehe za harusi kuliko watu wenye shida.

Mtoto Merrynes Benatus na mwenzake Anisia walizaliwa kituoni hapo January 29, 2018 wakiwa wameungana na baadae pacha huyo kufariki dunia baada ya kuanza kutapika akiwa kwenye usafiri wa ndege ambapo hali ilibadilika na kusababisha tumbo kuanza kuvimba ndiyo akafanyiwa upasuaji kuangaliwa tatizo ambapo hali ilibadilika na kusababisha kifo chake.

Kushoto ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Misenyi mkoani Hassan Moshi na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Misenyi, Rehema Mtawala (katikati) wakipokelewa na Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya cha St. Therese ,Francisca Francis (kulia). Picha zote na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya cha St. Therese ,Francisca Francis (kulia).

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Misenyi mkoani Hassan Moshi na katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Misenyi, Rehema Mtawala wakiwa na mama wa mtoto pacha Bi Jonesia Jovitus akiwa na mwanae Merrynes.

Mama wa mtoto pacha Bi Jonesia Jovitus akiwa na mwanae Merrynes wodini.

Mama wa mtoto pacha Bi Jonesia Jovitus akiwa amebeba mwanae Merrynes.

 Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Misenyi, Rehema Mtawala akiwa amemba mtoto Merrynes.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Misenyi mkoani Hassan Moshi akiwa amembeba mtoto Merrynes.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527