KITUO CHA UCHENJUAJI DHAHABU JEMA AFRIKA CHAPEWA ONYO LA MWISHO

Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa Onyo la Mwisho la Kukifungia Kituo cha Uchenjuaji Dhahabu cha Jema Afrika kilichopo Wilayani Kahama.

Hatua hiyo inafuatia kubainika kwa jaribio la wizi wa dhahabu uliofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa  kituo hicho kutaka kuiba dhahabu ya mteja.

Akizungumzia tukio hilo, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa kituo hicho kuandika barua ya kuweka makubaliano na Serikali ya kutojirudia tena kwa vitendo  vya wizi kituoni hapo.

‘’Ni jicho la huruma tu  tukiwapeleka mahakamani mali zenu zitataifishwa. Tunajua mmewekeza mitaji yenu na mna mikopo.  Nilishamwambia mmiliki kuwa kituo  chako kina rekodi ya wizi. Rais anawapenda, anawapigania ili watanzania wamiliki uchumi wa madini lakini mnamuangusha kwa kutofuata taratibu,’’ amesisitiza Waziri Biteko.

Amewatahadharisha wamiliki wa vituo vya uchenjuaji nchini kuhusu wizi wote wa dhahabu  unaofanyika na kuwasisitiza kwamba, unafahamika na kuwataka  wote wanaojihusisha na vitendo hivyo  kujiepusha  na  kwa wale wasiotaka kufanya kazi zao kwa  uaminifu watafute biashara nyingine.

Mbali na kutembelea kituo hicho,  pia, Waziri Biteko  na ujumbe wake  wametembelea Kituo Kidogo cha  Ununuzi   wa dhahabu kilichopo katika eneo la Wachimbaji wadogo wa Mwime  ambapo amewapongeza kwa kufuata taratibu na Sheria na kuwataka kufanya kazi zao kwa amani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  Zainab Taleck amesema  Mkoa huo unahitaji wawekezaji lakini walio waaminifu.

Ameongeza kuwa, wizi na udanganyifu katika kiwand cha uchenjuaji Jema Afrika ulibainiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kutumia fursa hiyo kuwatahadharisha wote wasiofuata taratibu kuwa serikali inawaona na itawafikia.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko pia ameongozana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Watalaam kutoka Tume ya Madini.

Aidha, ziara hiyo imefanywa wakati ambapo wizara na wadau wengine wa madini wanashiriki Maonesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Mkoani Geita yanayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 29, 2019.

Ziara hiyo imefanyika Septemba 28, 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527