BENKI KUU YA TANZANIA YAZITOZA FAINI BENKI TANO ZA BIASHARA KWA KUKIUKA KANUNI ZA KUZUIA UTAKATISHWAJI WA FEDHA HARAMU


Benki Kuu ya Tanzania imezitoza faini benki tano za biashara kwa kukiuka kanuni namba 17, 22 na 28 za Kanuni za Kuzuia Utakatishwaji wa Fedha Haramu za mwaka 2012 kwa kushindwa kuhakiki taarifa za utambulisho wa wateja na kushindwa kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka katika Kitengo cha Kuzuia Fedha Haramu (FIU). Benki hizo na kiasi cha faini ni kama ifuatavyo:


1.African Banking Corporation (T) Limited TSH 145 milioni 2. Equity Bank (Tanzania) Limited TSH 580 milioni 
3. I&M Bank (T) Limited TSH 655 milioni 
4. UBL Bank (T) Limited TSH 325 milioni 

5. Habib African Bank Limited TSH 175 milioni

Pamoja na faini hizo, Benki Kuu ya Tanzania imezitaka benki hizo kutekeleza yafuatayo ndani ya kipindi cha miezi mitatu toka tarehe faini zilipotozwa:

  1. Kupitia upya taarifa za wateja wao na kuhakikisha kwamba zinakidhi matakwa ya kisheria na kanuni zilizopo za uhakiki wa utambulisho wa wateja (KYC);
  2. Kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka ambayo ilitakiwa kuwasilishwa FIU;
  3. Kufanya tathmini ya ubora wa mifumo ya ndani ya kibenki na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa mifumo hiyo ipo madhubuti kwa lengo la kukinga mapungufu hayo hayarudii tena; na
  4. Kuwachukulia hatua stahili za kinidhamu, wafanyakazi wote waliohusika kufanikisha ufunguaji wa akaunti za amana kinyume na kanuni za kumtambua mteja (KYC).
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuzikumbusha benki na taasisi za fedha kuhakikisha kuwa zinafuata sheria na kanuni zilizopo nyakati zote. 


BENKI KUU YA TANZANIA 

botcommunications@bot.go.tz 
19 SEPTEMBA 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527