RAIS MAGUFULI AWAVAA TENA VIONGOZI WA MKOA WA DAR ES SALAAM " YANAFANYIKA MAMBO YA HOVYO, HUWEZI KUAMINI KAMA KUNA VIONGOZI KWENYE HUU MKOA"

Rais Magufuli amesema mambo ya hovyo  yanayofanyika katika mkoa wa Dar es Salaam yanamfanya ajiulize kama mkoa huo kuna viongozi.



Magufuli aliyasema hayo jana Jumapili Septemba 22, 2019 wakati akiwaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam viongozi mbalimbali aliowateua Ijumaa iliyopita ya Septemba 20,2019.

Miongoni mwa miradi ambayo Rais Magufuli ameonyesha kutoridhishwa nayo ni ya uboreshaji wa ufukwe wa Coco uliopo Manispaa ya Kinondoni.

Meya wa Manispaa hiyo ni Benjamin Sitta na mkuu wa wilaya hiyo ni Daniel Chongolo huku mkoa huo ukiongozwa na Paul Makonda.

Magufuli amehoji kitendo cha Meya wa Manispaa hiyo kumkabidhi mkandarasi mradi huo wa Coco ambao unaingiliana na ujenzi wa barabara inayopita baharini ya Salender.

Rais Magufuli aliwachambua viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakati akijenga hoja kuhusu viongozi wa mkoa wa Morogoro walioshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo na kuwataka viongozi wenye dhamana kuwatumikia wananchi wanaowaongoza.

Alisema Dar es Salaam yanafanyika mambo ya hovyo, huwezi kuamini  kama kuna viongozi, "Baada ya kutembelea machinjio ya Vingunguti, siku moja baadae nimeona kwenye TV Meya anakwenda kumkabidhi Mkandarasi site, ni mambo ya ajabu, Meya na kukabidhi site kwa Mkandarasi ni wapi na wapi? Mkandarasi mwenyewe ni yule aliyejenga soko la Mwanjelwa na akashindwa"

Rais Magufuli ameeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, huwezi ukajenga muundo mkubwa ndani ya mita 60 kutoka baharini au ziwani, lakini chakushangazwa alipokabidhiwa kuna mradi mwingine wa ujenzi wa daraja la Salender.

“Mradi huu wa Salender una barabara nne kuna nyingine inatoka Hospitali ya Aga Khan inapita katika daraja inakwenda hadi Coco Beach. Kibao kipo sasa unajiuliza miradi yote ni ya Serikali, huu mradi ,mkubwa tulitoa Sh200bilioni utapita wapi?

“Je watajenga muundo wa hoteli pale, je wale wachuuzi watafukuzwa. Mradi wowote ambao ni positive kwa watu lazima uwatafutie njia mbadala, lazima uwapeleke mahali ili mradi ukikamilika warudi,” amehoji.

Amesema Coco Beach haiwezi kujengwa kwa Sh14 bilioni, wakati kinachotakiwa ni kutengeneza njia sanjari na  kuweka vitu vya kukalia  kuwapa fursa ya watu wanaotaka ufukweni, kumpumzika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527