WAZIRI KABUDI AFUNGUA RASMI KIKAO KAZI MAALUM CHA MABALOZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje kuongeza jitihada katika kuhamasisha wawekezaji, wafanyabiashara na watalii kuja nchini ikiwa ni utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.Waziri Kabudi ameyasema hayo  tarehe 20 Agosti 2019 wakati akifungua rasmi kikao kazi maalum cha Mabalozi kinachofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere kuanzia tarehe 20 hadi 23 Agosti 2019.

Mhe. Waziri Kabudi alisema kuwa, Mabalozi ambao wana jukumu kubwa la kusimamia maslahi ya nchi kwenye nchi mbalimbali duniani, wameendelea kufanya kazi nzuri katika katika kuhakikisha dhana ya diplomasia ya uchumi inafikiwa na kwamaba matokeo ya jitihada hizo ni pamoja na kuongezeka kwa watalii, wawekezaji na wafanyabiashara nchini. P.ia kuongezeka kwa fursa za ufadhili wa masomo na ajira kwa Watanzania kwenye nchi mbalimbali

“Hii ni mara yangu ya kwanza kukutana nanyi Waheshimiwa Mabalozi tangu niteuliwe na Mhe. Rais kwenye wadhifa huu. Nazipongeza jitihada zenu katika utekeelzaji wa diplomasia ya uchumi kwani matokeo tunayaona kwa biashara kuongezeka hapa nchini watalii na hata wawekezaji. Hivyo nataka mwongeze jitihada Zaidi ili nchi yetu ifikie azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025” alisema Mhe. Kabudi”.

Aidha, Mhe. Waziri Kabudi alitoa rai kwa Mabalozi kuendelea kuwahamasisha Watanzania waishio nje (Diaspora) kujiandikisha na kuanzisha jumuiya zao ili kwa namna moja au nyingine na wao washiriki kuchangia maendeleo hapa nchini.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili Mabalozi hao ikiwa ni pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo ya balozi, Mhe. Kabudi alieleza kuwa Wizara inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi, Kiongozi wa Mabalozi hao, Mhe. Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Mabalozi walipata fursa ya kuitembelea. Alisema kuwa, miradi hiyo ni chachu ya maendeleo katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati. Tumepata fursa ya kujionea miradi hiyo ikiwemo ile ya ujenzi wa barabara, reli na umeme. Kimsingi miradi hii inalenga kumwondolea umaskini Mtanzania kwa vile itarahisha usafirishaji na kumwezessha mkulima kusafirisha kwa urahisi mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kupitia miundombinu hiyo.

Pia aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kufanikisha Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanyika nchini kwa mafaniko makubwa.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
20 Agosti 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post