WAFANYABIASHARA WASHAURIWA KUWEKEZA KWENYE VIWANDA VYA MAFUTA YA KULA NA SUKARI

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Wafanyabiashara nchini Tanzania na nje ya nchi wametakiwa kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa mazao mbalimbali yakiwemo miwa na alizeti.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 6 Agosti 2019 wakati akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la fursa za Kilimo biashara katika viwanja vya Nyakabindi kwenye maonesho ya Sikukuu ya wakulima (Nanenane) katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

Mhe Hasunga amesema kuwa endapo wakulima watawekeza katika Kilimo cha alizeti ni wazi kuwa wataimarisha upatikanaji wa mafuta ya kula yanayotokana na zao hilo hivyo kuondokana na dhana ya uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa Tanzania inauhitaji wa mafuta ya kula kiasi cha Tani 570,000 lakini pamoja na kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba lakini juhudi za uzalishaji bado ni ndogo kwani kama nchi inazalisha Tani 250,000 pekee.

Alisema kuwa kiasi cha Bilioni 678 zilitumika mwaka 2018 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ilihali kuna uwezo wa kuzalisha kwa wingi zao hilo na fedha ambazo zinatumika kuagiza  zingeweza kutumika katika kutekeleza miradi mingine.

Kuhusu Sukari, Waziri huyo wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa Tanzania ina uhitaji wa sukari kiasi cha Tani 675,000 ambapo Tani 175,000 kati ya hizo ni sukari za viwandani ilihali kiasi kilichosalia ni sukari ya kawaida, lakini uwezo wa nchi ni kuzalisha Tani 359,000 pekee.

Alisema kuwa ni jambo la ajabu kuagiza sukari nje ya nchi  kwa kutumia gharama kubwa ilihali kuna maeneo mazuri kwa ajili ya kilimo na kuzalisha miwa.

Aidha, amewasihi wakulima kuzalisha miwa kwa wingi kwani ni miongoni mwa mazao yanayohitajika zaidi katika biashara sambamba na kufanya mabadiliko katika sekta ya Kilimo kupitia mkazo wa Programu ya kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II).

Kongamano hilo la fursa za Kilimo biashara katika viwanja vya Nyakabindi kwenye maonesho ya Sikukuu ya wakulima (Nanenane) katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu limefunguliwa na Waziri Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya nne ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa Mhe Mizengo Peter Pinda.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527