TAASISI YA UHASIBU TANZANIA (TIA) KUBORESHWA KUENDANA NA MPANGO WA MIAKA MITANO


Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imeahidi kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) ili kuongeza udahili wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na  kupatikana kwa wahasibu wa kutosha kama mpango wa Taifa wa miaka mitano ulivyoelekeza.


Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipang,o Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa ziara yake ya kikazi katika taasisi hiyo iliyochini ya Wizara ya  Fedha na Mipango  kubaini changamoto za utekelezaji wa Bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka 2018/19.

Dkt. Kazungu alisema kuwa Taasisi ya TIA inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufinyu wa bajeti jambo lililosababisha baadhi ya miundombinu yake kutokamilika kwa wakati na hivyo kupunguza kiwango cha udahili wa wanafunzi.

“Lengo la Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano ni pamoja na taifa kuzalisha wahasibu wa kutosha ili kuleta chachu katika maendeleo ya uchumi na nyanja zingine za maendeleo, malengo yanayotegemewa kwa kuimarishwa kwa miundombinu ya taasisi hii”, alieleza Dkt. Kazungu

Alisema kuwa miundombinu inayoangaziwa kwa mwaka huu wa fedha ni pamoja na Mabweni ya wanafunzi, vyumba vya madarasa na ofisi za watumishi, aidha kuangalia uwezekano wa kuongeza wahadhiri kulingana na kozi zinazotolewa jambo litakalokwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji wa Taasisi ya TIA Bi. Luciana Hembe, alieleza  kuwa, hatua ya viongozi wa juu kutembelea taasisi wanazoziongoza na kuona uhalisia wa mambo, unaongeza morali ya kiutendaji ya watumishi kwa kuwa hutatua changamoto nyingi hususani za kibajeti.

Alisema kuwa Taasisi ya TIA imejipanga kikamilifu kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na weledi wa kutosha katika kuhimili ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post