LUGOLA ATAKA JESHI LA POLISI LITENDE HAKI KWA WANANCHI

Na Felix Mwagara, MOHA, IRINGA.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili mjini Iringa leo, na kulitaka Jeshi la Polisi Mkoani humo kutenda haki katika utendaji wao.

Lugola alifanya ziara ya saa mbili mkoani humo, akiwa safarini kuelekea Mkoa wa Rukwa kwa ziara ya siku tano mkoani humo.

Akizungumza katika kikao cha viongozi wa Polisi wa Mkoa huo, Lugola alisema amefika kuonana na viongozi hao akiwa safarini, kwa lengo la kufuatilia utendaji kazi ikiwa ni utaratibu wake ambao alijiwekea tangu aiongoze Wizara hiyo.

Lugola alisema lengo la ziara yake mkoani Rukwa ni kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake, na pia atafanya ziara kama hizo mikoa yote nchini.

Alisema anatarajia kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo kusikiliza kero za wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara itakayofanyika katika wilaya hizo.

“Natarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Agosti 10, 2019  Mjini Sumbawanga kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, kupokea taarifa ya Kamati hiyo, kabla ya kuanza kuzungumza na Wakuu wa vyombo vyake na baadaye kukutana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa, na kumaliza kwa kuzungumza na Baraza la Askari na Watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo mjini humo,” alisema Lugola.

 “Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Mji wa Sumbawanga, utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa mji huo wajitokeze kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia, na pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” alisema Lugola. 

Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma na mwezi Januari Mwaka huu Mkoa wa Kagera, Arusha Mwezi Februari na Morogoro wiki iliyopita, amegundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia Polisi wakiwaonea.

“kupitia kikao hiki hapa Iringa, napenda kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi, wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Rais Dokta John Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola.

Waziri Lugola baada ya kumaliza ziara yake Mjini Sumabwanga, ataenda Wilaya ya Sumbawanga Vijiji ambapo atatembelea Gereza Mollo kutatua mgogoro wa ardhi na baadaye atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.

Waziri Lugola, Agosti 12, 2019, atafanya ziara Wilayani Kalambo, na baada atamaliza ziara yake Wilaya ya Nkasi kwa kutembelewa majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini. 

Katika Wilaya zote atakazozitembelea pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.

Maagizo aliyoyatoa Waziri Lugola mara baada ya kuteuliwa kuiongoza Wizara hiyo, ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia alipiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

Pia aliagiza wakuu wa vyombo kuthibiti rushwa katika taasisi wanazoziongoza, na kutowanyanyasa watumishi katika taasisi zao.

Lugola anatarajia kumaliza ziara yake Agosti 17 mkoani humo na kurejea Dodoma kushiriki vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post