BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AFDB) KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA


Na. Saidina Msangi na Josephine Majura WFM Dodoma.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini chini ya ufadhili wa benki hiyo ambayo imekuwa na ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kanda ya Mashariki Bw. Gabriel Negatu alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)  katika ofisi  Wizara ya Fedha  na Mipango Jijini Dodoma.

Bw. Gabriel ameeleza kuwa Tanzania ni nchi ya mfano ambayo imeonesha matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi ya mbalimbali ya  maendeleo.

Akizungumza katika hicho Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa namna inavyowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Dkt. Mpango aliitaja baadhi ya miradi ambayo Benki hiyo imekuwa ikifadhili ni pamoja na  Sekta ya Miundombinu, Usafirishaji na Nishati ambayo kwa pamoja inachangia katika utekelezaji wa kujenga uchumi wa viwanda.

Aidha Waziri Mpango aliongeza  kuwa Sekta ya Nishati ni muhimu kwa nchi za Afrika kwani inahitajika kwa kiasi kikubwa katika kujenga uchumi wa viwanda kwani hakuna viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika katika ukuaji wa Sekta ya Viwanda.

Dkt.  Mpango alifafanua  namna ya  upatikanaji wa umeme vijijini kupitia REA umesaidia katika kuwezesha wananchi kupata habari mbalimbali na pia kujifunza teknolojia na kuona maendeleo katika maeneo mengine.

Benki hiyo inatarajia kufadhili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuunganisha Tanzania na Rwanda ambayo itachochea maendeleo  baina ya nchi hizo na Afrika Mashariki kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post