NAIBU WAZIRI WA MAJI, JUMA AWESO AAGIZA WATUMISHI WATATU WAKAMATWE NA WAFUKUZWE KAZI


Naibu waziri wa maji, Juma Aweso ameagiza kukamatwa na kufukuzwa kazi watumishi watatu wa mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( Muwasa) mkoani Mara kwa tuhuma za kuhujumu mamlaka hiyo.

Aweso alitoa agizo hilo mjini Musoma mkoani Mara jana Jumanne Agosti 6, 2019  wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji katika manispaa ya Musoma.

Watumishi hao ambao baada ya agizo hilo waliwekwa chini ya ulinzi na polisi ni pamoja Meshack Marco, Ramadhan Evarist na Jonas Paschal.

Aweso alisema katika ukaguzi huo amebaini watumishi hao pamoja na wengine ambao bado hawajatambuliwa wamekuwa na tabia ya kuwaunganishia maji wateja na kukusanya ankara za maji kila mwezi kinyume cha utaratibu.

"Nimekwenda Nyakato kuna mama alitoa Sh210,000 ili aunganishiwe maji na pesa hizo alipewa mtumishi anaitwa Rosta Kusaga lakini pesa iliyopelekwa kwenye mamlaka ni Sh 23,000 tu," alisema Aweso

Alisema mbali na vitendo hivyo lakini watumishi hao wamekuwa vinara wa kutunga uongo ili uongozi wa mamlaka hiyo uonekane mbaya  jambo ambalo alisema sio zuri kwa maslahi ya wakazi wa Musoma wanaotegemea mamlaka hiyo.

Alitolea mfano wa barua iliyoandikwa kwa pamoja na watumishi hao kwenda kwa waziri  wa maji huku wakidai mkurugenzi wa mamlaka hiyo amekuwa akitoa ajira kwa misingi ya ukabila wakidai robo tatu ya watumishi wa mamlaka hiyo ni kabila moja na mkurugenzi huyo jambo ambalo alisema kutokana na uchunguzi alioufanya amegundua kuwa sio kweli.

"Kuhusu suala la watumishi na maslahi yao nimeagiza muhusika wa masuala ya watumishi kutoka wizarani aje hapa aweze kupitia malalamiko ya watumishi ili kila mmoja aweze kupata stahiki zake maana hatutaki kumuonea mtu ila pia hatuko tayari kumvumilia mtu anayehujumu mamlaka," alisema Aweso


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527