NAIBU WAZIRI WA ARDHI DKT MABULA AAGIZA MASHAURI YA ARDHI KUISHA NDANI YA MIAKA MIWILI


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaagiza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini kuhakikisha Mashauri ya ardhi yanasikilizwa na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu shauri kufunguliwa katika Baraza.

Dkt. Mabula ametoa agizo hilo jana tarehe 6 Agosti 2019 katika eneo la Dongobesh wilayani Mbulu mkoa wa Manyara wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbulu mkoani humo.

Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora inayotolewa kwa weledi na uadilifu hivyo ucheleweshaji wowote wa mashauri unasababisha wananchi kushindwa kupata haki kwa wakati.

Aliwakumbusha watumishi wote wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutimiza majukumu yao kwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na ile itakayokuwa inatolewa ili kuboresha utoaji huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya katika kushughulikia mogogoro inayotokana na matumzi ya ardhi inalo jukumu la kuyapatia Mabaraza Watumishi ili yaweze kutekeleza majukumu yake vizuri.

‘’Mabaraza ya Ardhi yalikuwa yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa wenyeviti ambapo katika kukabiliana na changamoto hiyo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imeajiri wenyeviti wapya ishirini kwa ajili ya kuongeza nguvu kazi kwenye maeneo yenye migogoro mingi ya ardhi ikiwemo wilaya ya Mbulu’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia alizitaka halmashauri zote nchini kuhuisha Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji kwa yale yaliyomaliza muda wake na kutoa elimu au semina kwa wajumbe wa Mabaraza hayo kuwafahamisha majukumu yao.

Aidha, alisema idadi ya migogoro inayotokana na matumizi ya ardhi imeendelea kuongezeka siku hadi siku na kuwaasa wananchi wa Mbulu kutumia huduma za Baraza lililozinduliwa na kufuata taratibu za utatuzi wa migogoro inayotokana na matumzi ya ardhi ili kupata ufumbuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo alisema uanzishwaji wa Baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Mbulu umejibu kiu ya wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa Baraza hilo litasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri uliopo katika Baraza la Babati lakini pia litawarahisishia wananchi wa Mbulu kupata huduma iliyo karibu zaidi.

Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini mkoani Manyara Flatei Massey na Yule wa Mji Zakaria Isaay wameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuanzisha Baraza la Ardhi na Nyumba katika wilaya hiyo na kueleza kuwa Baraza hilo litawasaidia wananchi wa Mbulu mkoani Manyara waliokuwa wakitembea umbali mrefu wa kilomita 120 kufuata huduma ya Baraza katika wilaya ya Babati.

Hata hivyo, Wabunge hao walisema matatizo ya Ardhi katika wilaya ya Mbulu hayawezi kuisha iwapo jitihada za kupima ardhi ya wilaya hiyo haitafanyika na eneo kubwa la wilaya hiyo halijapimwa.

Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbulu lililozinduliwa linakuwa Baraza la nne katika mkoa wa Manyara wenye wilaya tano. Mabaraza mengine ni Simanjro, Babati na Kiteto.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amevitaka vijiji vyenye fedha katika wilaya ya Mbulu kuchangia fedha kwa ajili ya kufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Dkt Mabula alisema vijiji vyote katika wilaya hiyo ambavyo havina mpango wa matumizi bora ya ardhi vichukue hatua hiyo ili kuepusha migogoro ya wafugaji na wakulima na kubainisha kuwa iwapo zoezi hilo litafanyika maeneo katika vijiji hivyo yatajulikana kulingana na matumizi  yake na kusisitiza kuwa hapo migogoro haitatokea tena.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa kauli hiyo kutokana na kutoridhishwa na kasi ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji vya wilaya ya Mbulu ambapo kati ya vijiji 449 ni vijiji 145 pekee ndivyo vyenye Mpango huo jambo linalosababisha migogoro ya ardhi kuendelea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post