MKUTANO WA SADC WAHITIMISHWA, RAIS MAGUFULI ATAJA MAMBO WALIYOKUBALIANA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa SADC, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa wamekubaliana mambo kadhaa katika kikao cha wakuu wa nchi 16 kilichofanyika jana jioni Ikulu jijini Dar es salaam yakiwamo suala la kuondolewa kwa vikwazo kwa Zimbabwe, kufuatilia hali ya usalama nchini Congo na ombi la Burundi kujiunga na jumuiya hiyo.

Mengine ni kuwekeza kwenye miundombinu itakayowezesha kukua kwa uchumi katika ukanda wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, kuwa na chombo cha kukabiliana na majnga na suala la upatikanaji wa mapato.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano huo wa SADC wa siku mbili uliomalizika leo Jumapili Agosti 18, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa hotuba ya kuhitimisha mkutano huo, Rais Dk. John Magufuli amesema wakuu wa nchi wamekubaliana kuendelea kufuatilia hali ya usalama nchini Congo lakini pia wameiagiza sekretarieti kuharakisha chombo cha kukabiliana na majanga kitakachosaidia nchi wanachama kukabiliana na majanga kama vile njaa, mafuriko, vimbunga, magonjwa ya mlipuko na mengineyo.

Amesema katika mkutano huo pia, wakuu wa nchi walipitia hali ya uchumi katika ukanda wao ambapo uchumi wa nchi hizo ulishindwa kukua kama ulivyotarajiwa kwa asilimia saba na kushuka hadi asilimia 3.1, hivyo wamekubaliana kuwekeza kwenye miundombinu kwa kuwa ni mojawapo ya kikwazo cha kukua kwa uchumi kwenye bara la Afrika ikiwamo nchi za SADC.

Pamoja na mambo mengine, amesema mkutano huo pia umepitisha mpango wa kuongeza mapato kwa SADC ambapo nchi wanachama zitakuwa na hiyari ya kuchagua njia bora ya kuchangia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527