MALINZI ATOA UTETEZI WAKE MAHAKAMANI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (59), amedai mahakamani kuwa wakati anaingia madarakani shirikisho hilo lilikuwa na hali ngumu kiuchumi iliyosababisha madeni makubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha akaunti zake kufungwa kila wakati na kusema kuwa siku chache kabla ya kukamatwa, aliikopesha TFF Sh. Milioni 15.


Malinzi alitoa madai hayo jana wakati akijitetea dhidi ya mashtaka ya kughushi na kutakatisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Richard Rweyongeza, Malinzi alidai hali hiyo ilikuwa ikimlazimu kuikopesha TFF fedha zake binafsi na alikuwa akifanya hivyo kupitia akaunti waliyoifungua kati yake na shirikisho hilo.


 Amedai kiasi hicho cha sh. Milioni 15, zilikuwa ni kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa kufuzu fainali za Afrika kati ya Tanzania na Lesotho

Amedai akiwa Rais, alihakikisha shughuli mbalimbali za timu zinakwenda hadi kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa ambapo ili kufanikisha hilo, mara nyingine ilikuwa ikimlazimu kutumia fedha zake za mfukoni ili kuweza kuinusuru TFF .

Malinzi alidai kuwa aliikopesha TFF kutokana na hali ngumu ya kifedha iliyokuwa ikiikabili na hivyo kulazimika kutumia fedha zake binafsi, kukopa kwa watu binafsi ama kamati ya utendaji ili kunusuru hali hiyo hasa katika matukio muhimu yanayoikuta TFF na timu ya Taifa Taifa Stars.

Akiendelea kutoa utetezi wake, alidai, baadhi ya matukio ambayo alilazimika kutoa fedha zake na kuikopesha TFF mojawapo ni ile ya kulikomboa basi la TFF ambalo lilikuwa linashikiliwa na kampuni ya udalali ya Yono kufuatia amri ya mahakama la kuilipa Kampuni ya Pachi Line iliyokuwa ikitoa huduma za tiketi uwanjani.

Aliendelea kudai kuwa, aliilipa sh milioni 20 kwa kampuni ya udalali ya Yono ambapo TFF ilikuwa ikidaiwa na TRA na walitaka kukamata basi ambalo lilitolewa na wafadhili wao, Kampuni ya Bia ya TBL,Pia alilipia sh.milioni 40 za tiketi za ndege Kampuni ya Ethiopia Airline, za wachezaji wa Tàifa Stars waliokuwa wanakwenda Nchini Nigeria katika Mashindano ya Afrika yaliyokuwa yakufuzu Misri

Aidha aliongeza kudai kuwa aliwahi kuikopesha TFF USD 7000 wakiwa Harale, Zimbabwe baada ya wachezaji waTaifa Stars kutolewa mizigo yao nje ya hoteli waliyokuwa wamefikia kwa sababu Shirikisho la mpira Zimbabwe lilikuwa likidaiwa na hoteli hiyo,  na kusema hata baadhi ya mashahidi waliowahi kutoa ushahidi mahakamani hapa walithibitisha hilo akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa TFF Daniel Masangi.

Aliwataja mashahidi wa upande wa mashtaka waliodhibitisha jambo hilo Mahakamani akiwemo Katibu Mkuu Wilfred Kidao, Hellen Adam na Sareki Yonasi.Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Selestine Mwesigwa



Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 15 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya uwamuzi wa kupokelewa kwa kielelezo cha nyaraka ya taarifa ya madeni kati ya TFF na Malinzi ama la.


Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Selestine Mwesigwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527