KESI YA TUNDU LISSU KUPINGA KUVULIWA UBUNGE KUSIKILIZWA KESHO


Kesi ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, inatarajiwa kuanza kusikilizwa kesho.


Hati ya kuwaita pande mbili imetolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikiwaita wahusika kufika katika shauri hilo linalosikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Lissu alifungua shauri la maombi  Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo.

Mwombaji huyo anaomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu  alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.


Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amekuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kunusurika katika jaribio hilo la mauaji kwa takribani miaka miwili, tangu  Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527