KATIBU MKUU MIFUGO ASISITIZA UKUSANYAJI MAPATO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Profesa Elisante Ole Gabriel, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ili zitoe gawio serikalini.

Profesa Gabriel, ameyasema hayo jijini Dodoma katika kikao cha majadiliano kati ya wataalamu wa sekta za Mifugo na uvuvi na wataalamu kutoka taasisi binafsi ya Trade Mark East Africa yenye lengo la kusaidia uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia ya kielekroniki.

Amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inainuka kiuchumi kupitia kudhibiti mapato kwani kumekuwepo na upotevu mkubwa wa mapato uliotokana na kukosekana kwa njia imara za ukusanyaji.

Profesa Gabriel, ametolea mfano mnada wa Maswa ambao kabla ya udhibiti wa mapato ulikuwa ukikusanya sh. 756,000 kwa siku na baada ya udhibiti yameongezeka na kufikia sh. 7,028,000 kwa siku.

Kwa upande wa mnada wa Halmashauri ya Bariadi, mkoani Simiyu, Profesa Gabriel amesema kabla ulikuwa ukikusanya sh. Milioni 2,500,000 na baada yameongezeka hadi sh. 3,000,000 kwa siku na kufikia shilingi 14,950,000 kwa siku.

Aidha amewataka wataalamu hao baada ya kuwa na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato, pia kutafuta namna nyingine bora za kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato, akitolea mfano utalii kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi nchini.

Ameongeza kwa kusisitiza suala la elimu kutolewa kwa wafugaji na Wavuvi ambao ndiyo wadau wakuu wa sekta za mifugo na uvivu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark East Africa nchini, John Ulanga, amesema haijawahi kutokea katika taasisi zote walizofanya nazo kazi kuona utayari na ushirikiano kama walioupata kwa wizara ya mifugo na uvuvi.

Amesema lazima kuwepo na utayari wa kubadilika fikra katika utendaji ndani ya Wizara na taasisi zake vinginevyo mifumo hiyo haitakuwa na faida yoyote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post