TaCRI YAHAMASISHA WAKULIMA TARIME KUCHAKATA KAHAWA SAFI

Mkulima Mwita Hechei mkazi wa kijiji cha Mbogi kata ya Mbogi wilayani Tarime aliyeinama chini kuokota Kahawa akijaribu kuona ufanyaji kazi wa mashine aliyonunua sh.Milioni 1,900,000 kwa ajili ya kubangua Kahawa safi


Na Dinna Maningo  -Tarime  

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania Kituo kidogo cha Sirari Wilayani Tarime (TaCRI) imewataka wakulima wa Kahawa kuchakata kahawa safi kwani kwa kufanya hivyo watajiongezea kipato kikubwa cha fedha.

Akizungumza na wakulima wa zao hilo Meneja wa Kanda wa TaCRI Almas Hamadi alisema Wakulima wa Mara wengi wao huuza Kahawa ya maganda ambayo haiwapatii faida kubwa, hivyo wanapaswa kulima na kuuza kahawa safi iliyochakatwa ili kujipatia kipato kikubwa.

Hamadi alieleza kuwa, baadhi ya wakulima wameonyesha nia ya kuanza kuchakata Kahawa safi ambayo itawapatia faida ikilinganishwa na uuzaji wa Kahawa ya Maganda.

"Wakulima wabadilike waachane na mazoea ya kuuza kahawa yenye maganda sasa wanapaswa kuuza kahawa isiyo na maganda ambayo ni safi itawaingizia fedha nyingi.Nashukuru juhudi za TaCRI zimezaa matunda na mkulima mmoja wa kata ya Mbogi Mwita Hechei amenunua mashine ya kubangua kahawa safi",alisema Hamadi

Mmoja kati ya wakulima waliowezeshwa na TaCRI Joyce Petro alisema kwa kipindi chote walichokuwa wanauza kahawa ya maganda hawajawahi kuuza zaidi ya shilingi 1,400/= kwa kilo moja.

Mkulima wa Kijiji cha Nyarero Petro Bururyo alisema wameamua kuanza kuchakata kahawa safi baada ya kuona wakulima wenzao wa mikoa mingine kama Kilimanjaro wakiuza Kahawa safi kwa bei kubwa mpaka kufikia sh.4,000 kwa kilo.

Mwita Hechei aliyenunua mashine ya kubangua Kahawa kwa bei ya shilingi 1,900,000 alisema mashine hiyo itamsaidia kujipatia kipato lakini pia italeta ushawishi kwa wakulima wengine kuchakata na kuuza Kahawa safi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post