BOSI WA JAMII FORUMS ATETEA UHURU WA FARAGHA 'DATA ZA WATEJA MTANDAONI'


Na Fortune Francis - Mwananchi 
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo amedai sheria za kimataifa zinazoongoza mitandao zinataka wamiliki wa mitandao kuwa na sera ya faragha.

Melo na mwenzake Micke Wlliam wanakabiliwa na kesi namba 456 ya mwaka 2016 ya kuzuia Jeshi la polisi kufanya uchunguzi,

Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala jana Jumanne Agosti 6, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, Melo alidai kulingana na Katiba ya Tanzania Ibara ya 18 inalinda faragha ya mtu.

Alidai barua ya Februari 2, 2016 iliyosainiwa na Benedict Alex iliandikwa kwa niaba ya Jamii Media Co. LTD ilikuwa na majibu kwa Jeshi la Polisi.

Melo alidai katika majibu ya barua hiyo walieleza wapo tayari kutoa ushirikiano iwapo wataeleza ni kifungu gani cha sheria wametumia kinachowapa mamlaka ya kutaka data za wateja.

"Tuliahidi kutoa ushirikiano mkubwa endapo wangeeleza ni kwa mujibu wa sheria gani," alidai

Akiendelea kujitetea Melo alidai Jamii Forums ni mtandao wa kijamii ulioanzishwa Machi 2006 mwanzoni ukiitwa Jambo Forums ambapo unatoa nafasi ya mtu yeyote kujisajili na kutoa maoni yoyote kwa jina lolote

Aliendelea kudai katika uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Machi 8, 2017 na Jaji Korosso na Wenzake (Kitusi na Alfani) ambayo ni hukumu ya Kesi ya Jamii Media dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) ilieleza sheria hiyo wanaitambua na ili mtu kutoa taarifa wanatakiwa kuomba kibali cha Mahakama kabla ya kufungua kesi.

"Tulifungua shauri hili Mahakama Kuu baada ya kupata barua nyingi mfululizo kutoka Polisi na (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania) TCRA tukiiomba Mahakama isaidie kutafsiri barua hizo kwani tuliona haki ya faragha inaenda kuvunjwa," alieleza Melo

Melo aliiomba Mahakama ipokee hukumu hiyo kama kielelezo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali ya Tanzania, Sylvia Mitanto alipinga kupokelewa kwa kielelezo hicho kwa kuwa ni nakala na kuomba kupatiwa muda wa kutosha kwaajili ya kuipitia hukumu hiyo.

Hakimu Simba alieleza kesi hiyo itakapotajwa tena upande wa pili ulete majibu kuhusu pingamizi lililowekwa.

"Agosti 28 nitatoa uamuzi mdogo juu ya hili pingamizi na kuendelea na utetezi kesi yetu haitakiwi kuvuka Septemba 2019 kabla ya kutolewa hukumu," alieleza Hakimu Simba

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 28 na 29,2019 kwa ajili ya uamuzi mdogo na kuendelea na ushahidi.

Kabla ya utetezi mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, kinyume na Sheria Namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016 katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527